KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuondoka nchini keshokutwa kuelekea jijini Johannesburg, Afrika Kusini kukipiga na Bidvest Wits ya huko katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Jumamosi ijayo (Machi 12) saa 12.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa kwa sasa wanaipa mgongo kidogo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na wanahamishia nguvu zao zote kwenye mchezo huo dhidi ya Bidvest huku akiwaomba mashabiki wa timu hiyo waiunge mkono kwenye safari hiyo.

“Timu itaindoka Jumatano ijayo kuelekea Afrika Kusini, ambapo tutatengeneza faida ya kuwa jijini Johannesburg siku tatu kabla ya mechi, tunawaomba wapenzi na mashabiki wetu wote watuunge mkono kwenda huko na yoyote ambaye yuko tayari kuungana nasi kwenda Afrika Kusini, kwa Watanzania hakuna viza ya kuingia huko, kwa hiyo mtu yoyote ambaye yupo tayari amejipanga kwa nauli yake anaweza akaja akatusapoti tukiwa huko,” alisema.

Kawemba aliwahidi Watanzania na mashabiki wa Azam FC kuwa watacheza vizuri katika mchezo huo kama wanavyocheza hivi sasa katika ligi inayoendelea kutimua vumbi.

“Na matokeo ya Afrika Kusini tunaamini bado yatakuwa ni mazuri, uwezo wa uwanja ni mzuri tunaoenda kuuchezea ma kwetu sisi itakuwa ni faraja kwamba tunacheza kwenye uwanja mzuri na tunaweza kupata matokeo mazuri, tunashukuru tumecheza dhidi Yanga na hakuna majeruhi yoyote na Kavumbagu (Didier) amerudi kikosini akitoka kuuguza majeraha.

“Aggrey Morris yupo na anaweza akawa ni sehemu ya safari ya Afrika Kusini, lakini inategemea mwalimu atawatumia wahezaji gani, kwa hiyo tumesajili wachezaji 26 na wote wako vizuri kuelekea kwenye michuano hiyo,” alisema.

Mtaalamu huyo wa masuala ya uongozi wa soka, aliongeza kuwa lengo lao kubwa kwenye michuano hiyo ni kufika hatua ya robo fainali (hatua ya makundi) na wamejiandaa vya kutosha kuona kwamba wanavuka raundi hii na kuingia inayofuata.

Mara baada ya mchezo huo wa kwanza, Azam FC itarudiana na Bidvest baada ya wiki moja ndani ya Uwanja wa Azam Complex Machi 20 mwaka huu, itakayoanza kutimua vumbi kuanzia saa 9.00 Alasiri na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla kati ya timu ya Renaissance ya Chad na Esperance de Tunis ya Tunisia kwenye raundi ya pili itakayoanza kutimua vumbi Aprili mwaka huu.

Awashukuru Wakurugenzi na wadhamini NMB

Kawemba alimalizia kwa kuishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC na wadhamini Benki ya NMB kwa namna wanavyoendelea kutoa mchango wao kwenye timu hiyo mpaka sasa.

Mkwasa Kutangaza Kikosi Cha Taifa Stars
Abramovich Ajipanga Kumrejesha Lukaku