Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiomba Serikali na vyombo vya dola kwa ujumla kutoa taarifa za kina kuhusu hatua za mwisho za msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Ben Saanane asiyefahamika alipo.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu amesema kuwa hadi sasa chama hicho hakifahamu alipo Saanane na kwamba pamoja na jitihada za kumtafuta hospitalini, polisi hadi katika vyumba vya kuhifadhia maiti hawajafanikiwa kumpata.

Lissu aliliomba jeshi la polisi kutoa taarifa kama linamshikilia Saanane ama la. Aliongeza kuwa kama Jeshi hilo halimshikilii litoe taarifa za mwisho za mawasiliano yake kabla ya kutoweka.

“Katika mazingira haya, tunaiomba serikali na vyombo vyake vya ulinzi, ituambie kama imemkamata na inamshikilia Ben Saanane tuanzie hapo…lakini kama hawajamkamata na hawamshikilii, serikali na vyombo vyake watueleze mawasiliano yake ya mwisho yalikuwa lini, na nani, wapi na yalihusu nini,” alisema Lissu.

Lissu alisisitiza kuwa Serikali ndiyo yenye uwezo wa kudhibiti mipaka yote ya nchi hivyo wanaiomba ieleze endapo kiongozi huyo wa Chadema alitoka nje ya mipaka ya nchi.

Akizungumzia hatua za mwisho za mawasiliano ya Saanane ndani ya chama hicho, alisema Novemba 14 ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwake kuwasiliana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa Dodoma na tangu hapo hakuwahi kuwasiliana na kiongozi yoyote.

“Alimwambia mwenyekiti uko wapi, akamwambia nakwenda kwenye maziko ya Samuel Sitta, mawasiliano ya mwisho ni ya tarehe 14 Novemba,” alisema Lissu.

Lissu alisisitiza kuwa hakuna anayejua aliko Saanane ndani ya chama hicho kama baadhi ya watu wanavyosema na kwamba kama wangefahamu wangekuwa wameshasema alipo.

Saanane aliripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 18 mwaka huu.

Chelsea Wajitanua Kileleni
Wafuasi wa Lipumba na Maalim Seif wapigana tena mahakamani