Klabu za Arsenal na Chelsea zimetajwa kusalia katika mbio za kumuwania mshambuliaji kutoka nchini Hispania pamoja na klabu bingwa nchini Italia Juventus, Alvaro Morata.

Tovuti ya GianlucaDiMarzio.com, imeripoti kwamba klabu hizo mbili za nchini England, zitalazimika kutunishiana misuli katika mbio za kumsajili mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha Hispania katika fainali za mataifa ya barani Ulaya (Euro 2016) ambazo zinaendelea nchini Ufaransa.

Tayari imeshafahamika kwamba Morata, ataondoka katika kipindi cha majira ya kiangazi kufuatia dhamira yake ya kutaka kucheza soka nje ya nchini Italia, ambapo amedumu nchini humo kwa miaka mitatu sasa.

Chelsea wana mpango wa kumsajili Morata, ili kuongeze makali katika safu yao ya ushambuliaji ambayo imekua ikiongozwa na Diego Costa, lakini wakati mwingine hutokea changamoto ya kukosekana kwake uwanjani kutokana na adhabu ama majeraha.

Kwa upande wa Arsenal wanaendelea kuhaha na harakati za usajili wa mshambuliaji, kutokana na hitaji la kuongeza mtu kwenye safu ya ushambuliaji ambayo imekua ikimtegemea sana Olivier Giroud.

Majuma mawili yaliyopita The Gunners walionyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa klabu bingwa nchini England, Leicester City, Jamie Vardy lakini pamekua na hali ya sintofahamu kutokana na mshambuliaji huyo kutosema mustakabali wake kama ataendelea kubaki King Power Stadium ama kutimkia kaskazini mwa jijini London.

Wakati mipango wa kumpeleka Morata jijini London ikiendelea baina ya klabu hizo mbili, uongozi wa Juventus umetangaza dau la Pauni milioni 40, kama thamani ya mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa ameshakitumikia kibibi kizee cha Turin katika michezo 63 na kufunga mabao 15.

Mwakyembe kuliburuza mahakamani gazeti la 'Dira' kwa kuandika ametapeli bilioni 2
Video: Rais Magufuli ametaka kodi yake ikatwe ili kuongeza mapato ya serikali.