Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania (CWT), limewasimamisha uongozi Katibu Mkuu wa chama hicho, Deus Seif na mweka hazina, Abubakar Allawi.

Kaimu Rais wa CWT, Dinah Mathamani ameyasema hayo Jumamosi Septemba 17, 2022 alipokua akizungumzia uamuzi wa baraza hilo lililokutana kwa dharura kuanzia Septemba 15, 2022 hadi Septemba 17, 2022.

Katibu Mkuu wa chama CWT, Deus Seif

Mathamani amesema viongozi hao wamesimamishwa uongozi baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi sita kwa kutiwa hatiani kwa kosa la uhujumu uchumi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

“Baada ya Baraza la Taifa kupokea taarifa hiyo ya hokum ya mahakama na kujadili, wajumbe waliazimia kuwasimamisha Mwalimu Deus Seif na Abubakar Allawi katika nafasi zao za uongozi na utendaji ndani ya chama cha Walimu Tanzania wakisubiri maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Taifa,” amesema Mathamani.

Mweka hazina CWT, Abubakar Allawi

Amesema viongozi hao kwa kipindi chote ambacho wamesimamishwa hawatahusika na shughuli zozote zinazohusiana na CWT.

Juni 28, 2022 Seif na Allawi walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam kifungo cha miezi sita jela pamoja na kurejesha fedha za CWT Sh milioni 13.9 baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na uchepushaji wa fedha hizo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 18, 2022    
Ruto akataa wapinzani kwenye serikali yake