Aliyekuwa Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes Da Rosa, ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Mauritania.

Gomes mwenye umri wa miaka 52, ametangazwa kushika nafasi hiyo, baada ya Uongozi wa Shirikisho la soka nchinI Mauritania kumfuta kazi Corentin Martins hivi karibuni.

Martins alifutwa kazi kufuatia kushindwa kufikia lengo la kuivusha Timu ya Taifa ya Mauritania hadi hatua ya mtoano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, zitakazounguruma nchini Qatar.

Gomes anapata kazi baada ya kuondoka Simba SC majuma matatu, kufuatia kuvunja mkataba wake na Uongozi wa klabu hiyo.

Kocha huyo aliamua kuondoka Msimbazi, kufuatia kushindwa kufikia lengo la kuivusha Simba SC hadi hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kikosi chake kufungwa na Jwaneng Galaxy mabao 3-1 jijini Dar es salaam.

Kabla ya mchezo huo wa Mkondo wa pili, Simba SC ilishinda mabao 2-0 ugenini mjini Gaborone nchini Botswana.

Hata HIvyo Gomes aliyejiunga na Simba SC mwanzoni mwa mwaka huu 2021, ameiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho msimu wa 2020/21.

Red Arrows FC waanza kujihami
Wagonjwa wa Saratani waongezeka Kanda ya Ziwa