Bandari ya Dar es Salaam hivi sasa haipenyeki kufuatia usimamizi unaowatia mtegoni wajanja waliokuwa wanaiba mali ya umma na kuvusha kupitia bandari hiyo.

Jana, Wizara ya Maliasili na Utalii ilifanikiwa kukamata makontena 31 yaliyokuwa yamebeba magogo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 ambayo hayajaongezwa thamani, kinyume cha sheria ya Misitu ya Mwaka 2002.

Thamani hiyo ya shilingi milioni 300 inajumuisha makontena sita mengine yaliyokamatwa katika maeneo ya Rukwa, Mbeya, Kibaha na Mbezi jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kiintelijensia ziliwezesha Wizara hiyo kubaini mpango huo. Maafisa wake wakiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Adelhelm Meru walifika na kuwatia mbaroni watu waliokuwa wanasafirisha makontena hayo ya magogo kinyume cha sheria.

“Baada ya kupata hizi habari, tulikimbia hapa Bandarini kuja kuona haya makontena 31 yametoka wapi na yanakwenda wapi,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru.

Baada ya kuwahoji watuhumiwa, walieleza kuwa magogo hayo yalitoka nchini Zambia, hali iliyopelekea Ubalozi wa nchi hiyo kufika bandarini kubaini magogo hayo na kuyatolea ufafanuzi.

Baada ya kuyakagua magogo hayo, Naibu Balozi wa Zambia, Bi. Elizabeth Phiri aliwaeleza waandishi wa habari kuwa magogo hayo hayakutoka nchini Zambia kwa kuwa nchi hiyo hairuhusu biashara ya magogo ambayo hayajaongezwa thamani bali inaruhusu biashara ya mazao ya mbao.

Alisema hata kama kutakuwa na nyaraka zozote zinazooenesha kuwa magogo hayo yalitoka Zambia, bado itakuwa ni kinyume cha sheria ya Zambia hivyo nyaraka hizo haziwezi kuhalalisha kosa hilo.

Nyundo Ya Hapa Kazi Tu Yawaangukiwa Wengine Watatu TRA
Mkuu wa Mkoa Afuta Likizo za Watumishi Wote Mwaka Huu, Ataka Wachape Kazi Tu!