Kiungo Henrikh Mkhitaryan amelazimika kurejea Old Trafford akitokea kwenye kambi ya timu ya taifa ya Armenia baada ya kupata majeraha wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Jamuhuri Ya Czech uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo.

Taarifa za kuumia kwa kiungo huyo ambaye alijiunga na Man Utd mwezi Julai akitokea Borussia Dortmund ya nchini Ujerumani, zimeibua hofu ya kukosekana kwenye kikosi kitakachocheza mchezo wa ligi dhidi ya Man City mnamo Septemba 10.

Mkhitaryan mwenye umri wa miaka 27, aligongana na kiungo wa timu ya taifa ya Jamuhuri ya Czech Marek Sukhy katika dakika ya 37 ya mchezo huo, ambao ulishuhudia timu ya taifa ya Armenia ikifungwa mabao matatu kwa sifuri.

Licha ya kushindwa kupata nafasi ya kwenye kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa klabuni hapo, bado Mkhitaryan anapewa nafasi kubwa ya kuwa sehemu ya wachezaji ambao huenda wakapambana na Man city mwishoni mwa juma lijalo.

Mapema juma hili Jose Mourinho alionyesha hofu ya wachezaji wake kuwa katika hali nzuri kiafya pindi watakaporejea klabuni hapo, baada ya kumaliza majukumu ya kuzitumikia timu zao za taifa ambazo zipo katika harakati za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

Taifa Stars Yaelekea Nigeria
UVCCM yaivaa rasmi Chadema kwa kushindwa kufanya UKUTA