Serikali ya Iran imesema kuwa italipa kisasi dhidi ya tukio la kushambuliwa kwa vinu vyake vya nyuklia vya chini ya ardhi, ambalo imedai limefanywa na Israel.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Mamlaka ya Iran, vinu hivyo vya madini ya uranium vilivyoko Natanz vililengwa na mashambulizi ya kigaidi, Jumapili ya Aprili 11, 2021.

Ingawa Israel haijajibu kuhusu tuhuma hizo za Iran na mpango wa kulipa kisasi, vyanzo vya kiintelijensia vya Marekani vimeiambia New York Times kuwa madhara ya mashambulizi hayo yalikuwa makubwa kuliko yalivyoripotiwa na Iran.

Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa mashambulizi ya mabomu yaliteketeza kabisa mifumo ya umeme ya eneo hilo la kutengeneza nyuklia.

Imekadiriwa kuwa huenda ikachukua zaidi ya miezi tisa kwa serikali ya Iran kurejesha shughuli za utengenezaji wa nyuklia katika eneo hilo.

Hivi karibuni, Israel ilionya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, wakati ambapo kumekuwa na jitihada za kutaka kurejesha mazungumzo kati ya Iran na Marekani ya kurejesha ‘mpango wa nyuklia’(Nuclear Deal) uliosainiwa mwaka 2015.

Mpango huo ulikuwa umefikiwa na nchi hizo mbili pamoja na mataifa mengine sita yenye nguvu, ambapo Iran ilikubali kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli zake za nyuklia. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya Marekani na washirika wake kuiondolea Iran vikwazo.

Hata hivyo, baada ya kuingia madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump alivunja makubaliano hayo na kuweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran.

Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden amesema anataka kurejesha hali ilivyokuwa na kuhuisha makubaliano hayo ya mwaka 2015.

Hata hivyo, nchi hizo sita ambazo ni China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Uingereza zimemtaka Biden kuiondolea vikwazo Iran kwanza, na Iran kurejea kwenye kiwango cha chini cha uzalishaji wa nyukilia walichokubaliana.

Mtambo wa VAR kufungwa Uwanja wa Mkapa
Mtoto wa darasa la nne abakwa na kuuawa, atupwa ufukweni