Mawaziri Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye wameanza kufungua makucha yao rasmi wakitumia uzoefu walioupata ndani ya CCM kuijenga Chadema.

Wanasiasa hao ambao ni wajumbe wa kamati kuu ya Chadema, wamegawana mikoa ya Kanda ya Kati wakisaidiana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na viongozi wengine kupandikiza mbegu ya chama vijijini.

Utekelezaji wa mkakati huo unakuja ikiwa ni miezi michache baada ya Lowassa kuishauri Chadema kujijenga kama chama kinachojiandaa kukamata dola na kuacha uanaharakati, kwa kuhakikisha kuwa inajidhatiti katika maeneo yote hadi ngazi za mashina vijijini kama ilivyo CCM.

Akiwa ndani ya CCM, Lowassa anatajwa kuwa ‘mkali’ wa siasa za chinichini za kujijenga mijini na vijijini, mkakati ambao umeiwezesha CCM pia kuendelea kushinda kwa kishindo hasa katika maeneo ya vijijini.

Hivi karibuni, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema kuwa anaamini CCM itaendelea kuwa madarakani kwa miaka 20 mingine ijayo kwani imejidhatiti kwa kuwa na wawakilishi hadi ngazi ya nyumba kumi (mabalozi).

Akizungumzia ziara ya wanasiasa hao wakongwe, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Chadema, Tumaini Makene licha ya kueleza kuwa imelenga katika kufanya uchaguzi wa kanda ya kati wa Mwenyekiti, Makamu na Mweka hazina wake, alikiri kuwa wamebeba mkakati wa kujenga chama hicho.

“Kazi ya kujenga chama lazima ifanyike kwa mkakati mbalimbali,” amesema Makene.

Mpango wa kuanza mkakati wa kujijenga mjini na vijijini wa Chadema ulipitishwa rasmi katika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam na baadae kuwashirikisha wabunge wa chama hicho, Novemba mjini Dodoma.

Lissu Pasua Kichwa, Hakimu amuuliza Wakili wa Serikali ‘Mnamuogopa?’
Orodha Ya Wanaowania Tuzo Ya Bao Bora 2016