Jotoridi la siasa limewashinda madiwani wa CCM na wa vyama viwili vilivyo ndani ya Ukawa; Chadema na CUF ambao leo wameshambuliana kwa ngumi kwenye uchaguzi wa Naibu Meya wa Ilala jijini Dar es Salaam.

Ugomvi huo umezuka baada ya Chadema na CUF kudai kuwa kura zao zimechakachuliwa katika uchaguzi huo uliomalizika kwa kumtangaza mgombea wa CCM, Omar Kumbilamoto kuwa mshindi.

Kumbilamoto alitangazwa kutetea kiti chake akiwa na kura 27 akifuatiwa na Adam Rajabu (CUF) aliyekuwa na kura 25, huku mgombea wa Chadema, Patrick Assenga akiambulia patupu (0).

Imeelezwa kuwa chanzo cha vurugu hizo ni malalamiko kutoka kwa mgombea wa Chadema ambaye alikuwa ndani ya chumba maalum cha kuhesabia kura na baadaye kutoka akipiga kelele kuwa “CCM wameanza kuchakachua uchaguzi.”

Baada ya askari kuingia ndani ya chumba hicho cha kuhesabia kura, mgombea huyo wa Chadema alidai kuwa askari walimuamuru mgombea wa CUF kurudisha kura alizokuwa amehesabiwa mkononi zilizokuwa 27 na kwamba alipewa mgombea wa CCM, Kumbilamoto.

Baada ya matokeo kuonesha kuwa Kumbilamoto amepata ushindi wa kura 27, alitoka nje akiwa anashangilia, lakini alikutana na Assenga ambaye alikuwa na madiwani wa Chadema akiwasimulia yale aliyowaaminisha kuwa yametokea ndani ya chumba cha kuhesabia kura na ndipo pande hizo mbili zilipoanzisha ugomvi wa ngumi na matusi.

Chanzo: Mtanzania

Nicki Minaj amwaga machozi akieleza alivyonyanyaswa na wapenzi
Odinga, Ruto wamuweka njia panda Rais Kenyatta

Comments

comments