Rais John Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya operesheni maalum ya kukomesha wizi wa kazi za wasanii kupitia santuri zisizo na stika za Mamlaka hiyo.

Dk. Magufuli ametoa agizo hilo leo katika Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na wasanii na makundi mbalimbali yaliyomuunga mkono kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, kwa lengo la kuwashukuru.

“Nitoe wito kwa TRA, kama ambavyo wameweza kufanya kazi maeneo mengine… ya kushika makontena ambayo hayawezi kufichika, wafanye hivyo hivyo kwa operesheni maalum kwa kazi za wasanii ambazo hazina stika,” alisema Rais Magufuli.

Pia, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye kumuandikia barua Waziri Mkuu kumuomba airudishe kwenye wizara yake COSOTA ambayo hivi sasa iko chini ya wizara ya viwanda na biashara huku ikishughulikia masuala ya Haki Miliki za wasanii.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri (Nape), hili la kengine kuwa katika Wizara ya viwanda na biashara, kingine kiko wizara ya sanaa, kingine kiko wizara ya ulinzi, kingine kiko wizara ya mambo ya ndani, wakati vyote vinahusiana na wizara yako… mwandikie Waziri Mkuu,” Rais Magufuli aliagiza.

Rais Magufuli aliwaahidi wasanii, waandishi wa habari na wana michezo kuwa ataendelea kushirikiana nao kama ilivyokuwa wakati wa kampeni kwakuwa walianza wote na watamaliza wote.

Makundi hayo pia yalimshukuru Rais kwa mchango wake na kumuomba aendelee kuwasaidia katika kuondoa changamoto zinazowakabili, kubwa likiwa mfumo kukomesha wizi wa kazi zao pamoja na kuweka mfumo thabiti wa kusimamia kazi zao.

 

 

Ney wa Mitego aeleza kwanini hukataa show za Ulaya, amchana tena Ommy Dimpoz
Ajabu: Mfungwa ajidunga 'mimba' kukwepa adhabu ya kunyongwa