Ndoto, nia na matarajio ya kuwa rais wa serikali ya awamu ya tano inakaribia kutoa majibu kwa mgombea urais wa CCM, Dkt. John Magufuli saa chache zijazo huku akirusha kete yake ya mwisho.

Mgombea huyo ameonesha kuwasogelea zaidi watumishi wa umma huku akiwatoa wasiwasi kuhusu kile kinachodaiwa kuwa yeye ni mkali na huenda akawasumbua watendaji serikalini.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliofika katika viwanja vya Jangwani Dar es Salaam jana, Dkt. Magufuli alieleza kuwa atakuwa rafiki wa wafanyakazi na atawapigania ili waweze kupunguziwa makato ya kodi kwenye mishahara yao kwa kiwango kikubwa kutoka asilimia 11 inayowagusa wengi.

Hata hivyo, Dkt. Magufuli alisisitiza kuwa yeye hatawaonea haya wafanyakazi ambao wataenda kinyume na taratibu za kazi hususan wale wanaofanya ubadhilifu.

“Mfanyakazi Yule ambaye atakuwa amekula pesa ya umma Dar es Salaam, mimi sitamhamishia Mwanza, ataishia hapa hapa Dar,” alisema Dkt. Magufuli.

Alitaka wafanyakazi kumpigia kura ili akafanye nao kazi kweli kwa kuwa hata vitabu vya dini vimeandika ‘asiyefanya kazi asile’, hivyo atakuwa rafiki wa wafanyakazi lakini wachapa kazi kweli.

Aidha, Dkt. Magufuli aliwaahidi madereva kuwa atahakikisha anashughulia matatizo yao na watakuwa na mikataba ya kazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine hivi sasa nchini.

Pamoja na mambo mengine, mgombea huyo aliahidi kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la foleni katika jiji la Dar es Salaam kwa kujenga madaraja ya juu (fly overs).

Leo, Dkt. Magufuli pamoja na viongozi wengine wa CCM watafunga kampeni zao jijini Mwanza ambapo kwa mujibu wa mjumbe wa kamati ya kampeni ya chama hicho, January Makamba, ufungaji huo utakuwa wa kipekee na wa kihistoria.

 

Pape N’daw: Ninasingiziwa, Sikuvaa Hirizi
Mbadala Wa Kaseja Azungumza