Rais John Magufuli amewanyooshea kidole watu ambao wanakosoa mtindo wake wa kuwasimamisha kazi hadharani watumishi wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya kiutendaji.

Juzi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilieleza kuwa mtindo unaotumiwa kuwasimamisha hadharani watendaji bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza hauzingatii haki za binadamu.

Akiongea jana jijini Dar es Salaam na viongozi wa CCM ngazi za Mikoa na Wilaya, Rais Magufuli alisema kuwa waliotumia madaraka yao vibaya kuwaibia wananchi kwa miaka mingi wanastahili kuadhibiwa hadharani kwani wao pia waliwaibia hadharani wananchi hao.

“Kama haki za binadamu ziko kwa matajiri waliokuwa wanaiba, haki za binadamu hawa waliokuwa wanaibiwa hazipo?” Alihoji. “Kwa hiyo unaweza kuona hata wanaowatetea watu hao ni majipu na tutaanza kuwafuatilia,” alisema.

Alisema kuwa huu ni wakati ambao wao pia wanapaswa kuyapata mateso waliyoyapata Watanzania walio wengi kwa muda mrefu waliokuwa wakiibiwa na watendaji hao.

“Aliyewateua ni mimi na niliwataja hadharani, sasa kwa nini wafurahie kutajwa hadharani siku ya kuteuliwa na wasitajwe hadaharani siku ya kutumbuliwa. Hao ndio saizi yangu kuwatumbua. Kama ni Mkurugenzi wa Manispaa au wapi nimemteua mimi,”alisema Rais.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alimsimamisha kazi hadharani aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumpa maelezo ya udanganyifu alioufanya mtendaji huyo katika utoaji wa zabuni na usimamizi wa mkataba wa ukusanyaji tozo katika Stendi ya Ubungo. Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa yaliyojiri wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni alilolibatiza jina la ‘Daraja la Nyerere’.

 

Mwanamuziki Nguli wa Rock, Prince afariki, azidiwa na dawa za kulevya
Gumzo la Mshahara wa Rais Magufuli laibukia Bungeni, Mbunge wa Chadema amfananisha na Nyerere