Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za Binadamu, Michelle Bachelet ametoa wito kwa Serikali kuzingatia wajibu wao wa Kimataifa wa kulinda haki za Wananchi za haki ya kupata taarifa na kujieleza.

Bachelet ameyasema hayo hii leo Juni 19, 2022, wakati akihutubia mkutano wa 50 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu uliozungumzia kwa sehemu kubwa suala la taarifa za uongo na hatua sahihi za kuchukua ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Matatizo ya jamii zetu hayaanzi na taarifa za uongo, bali huchochewa na taarifa za uongo. Dalili zake ni kuenea kwa magonjwa yanayokabili dunia hivi sasa, mojawapo ni ukosefu wa usawa uliojikita kimfumo, ubaguzi, taasisi zilizo dhaifu, umma kupoteza imani kwenye mifumo ya utawala na ukosefu wa utawala wa sheria,” amesema Bachelet.

Amesema, taarifa za uongo ni zile ambazo mtu au watu wanasambaza wakijua ni za uongo na hazina ukweli wowote tofauti na taarifa potofu ambazo zimepindishwa kwa malengo ya wasambazaji na husambaa pindi watu wanapoona sauti zao hazisikilizwi na kutokuwa na imani na mifumo ya kisiasa, hali ya kiuchumi kuwa mbaya sambamba katika jamii.

“Na taarifa hizi zinashamiri pindi Mashirika ya kiraia, Waandishi wa Habari, Watetezi wa haki za Binadamu na Wanasayansi hawawezi kufanya kazi zao, hawawezi kukusanyika na kuzungumza kwa uhuru, uhuru wa kiraia umebinywa au kufungwa kabisa ikiwemo haki ya kupata taarifa, kuzungumza na kukusanyika zimesitishwa,” ameongeza Bi. Bachelet.

Hata hivyo, amesema “katika kukabili changamoto hizo hatupaswi hatupaswi kutumbukia kwenye mtego wa kujaribu kuamrisha kipi ni uongo na kipi ni sahihi kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kuziba kabisa fursa ya kidemokrasia.”

Kufuatia hali hiyo, Bi. Bachelet ametaka Serikali kujikita katika kutathmini ni vipi mifumo ya mawasiliano inabadilishwa na teknolijia na kuangalia ni kwa jinsi gani zinaweza kudhibiti changamoto zinazosababishwa na habari za uongo na wakati huo huo kushughulikia visababishi vya ukuaji wake.

Amesema, hatua za kisera za uandishi huru na kuimarisha uwepo wa vyombo vingi vya Habari ni muhimu katika kusaidia mtu au watu kujipambanua katika mifumo ya sasa ya habari, ikiwemo kuimarika kwa mifumo ya elimu ya kumwezesha mtu kufanya tafakuri ya kina ni muhimu itayosaidia katika mazingira ya sasa.

“Wale walio madarakani ambao wanaamua kusambaza taarifa za uongo ili kukandamiza taarifa ambazo hawapenzi kuzisikia au kuonea na kunyanyasa kauli zinazowakosoa, ni lazima wawajibishwe,” amesema Bachelet.

Aidha, amekumbusha kuwa kushughulikia changamoto ya taarifa za uongo si wajibu wa Serikali pekee, bali pia majukwaa ya mitandao ya kijamii ambayo nayo yamebadili upepo wa usambaaji wa taarifa kwenye jamii, hivyo kuwa na jukumu la utambuzi wa ni jinsi gani yatarekebisha ajenda ya Kitaifa na Kimataifa.

Simba SC yafafanua mkataba wa mwaka mmoja
TPLB: Kanuni zitaamua mfungaji bora