Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) amelazimika kutoka katika kikao cha baraza la madiwani, ikiwa ni hatua yake ya kupinga Kaimu Mtendaji wa kata ya Kipili, Justine Jordan, kukabidhiwa zawadi ya pikipiki akitaka chombo hicho cha usafiri kiwe mali ya Serikali na si ya mtu binafsi.
Tukio hilo limetokea kabla ya kuahirishwa kwa baraza hilo la madiwani lililoketi katika Mji wa Namanyere, wilayani Nkasi wakati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Sumuni Mwanakulya alipokuwa akimkabidhi Jordan pikipiki aina ya SNLG namba MC 611BNP ya thamani ya zaidi ya Sh milioni mbili.
Jordan ambaye pia ni Ofisa Ugani alizawadiwa na halmashauri ya wilaya hiyo pikipiki hiyo baada ya kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kata yake ambapo amekusanya zaidi sh. milioni 100 alizopangiwa.
Aidha, Mwenyekiti Mwanakulya alipolitangazia baraza hilo la madiwani kuwa halmashauri ya wilaya hiyo imeamua kumzawadia Jordan pikipiki hiyo, baadhi ya madiwani walihoji uhalali wa zawadi hiyo wakitaka isiwe mali ya mtu binafsi bali iwe mali ya Serikali, kutokana na hali hiyo, mbunge Keissy alisusa tukio hilo kwa kutoka ukumbini.
“Huyu mtendaji ametukusanyia zaidi ya Sh milioni 50 kati ya Sh milioni 100 aliyopangiwa, kumzawadia pipikipi ya thamani ya Sh milioni mbili imekuwa nongwa, hivi hizi roho za kwa nini zinatokea wapi? Pikipiki hii ni mali yake binafsi,” amesema Mwanakulya.
Hata hivyo, pamoja na mjadala kuibuka ukumbini kwa baadhi ya madiwani kutokubaliana na hatua ya mtendaji huyo kupewa pikipiki, madiwani wengine walimmwagia sifa Jordan kwa kuweza kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kata yake ya Kipili kwa uaminifu huku wakiwataka wengine waige mfano wake.

Video: Operesheni tokomeza viroba yazidi kushika kasi Jijini Dar
Mfanyabiashara aliyempa Makonda eneo ajibu tuhuma