Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mchungaji Peter Msigwa amekosoa hatua ya Rais John Magufuli kutohudhuria sherehe ya kufungua mwaka mpya iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wawakilishi wa kidiplomasia kutoka nchi mbalimbali.

Mchungaji Msigwa ambaye anahudhuria vikao vya kamati za Bunge jana jijini Dar es Salaam, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ni jambo la kushangaza kwa Mkuu wa nchi kutohudhuri sherehe hiyo muhimu wakati imefanyika Ikulu anapoishi.

“Ulikuwa utamaduni wa baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutumia mikutano kama hiyo kuwaambia wawakilishi wa kidiplomasia msimamo wa nchi na aina ya uhusiano ambayo nchi yetu inapenda kuujenga na dunia,” alisema Mchungaji Msigwa.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDS), Dk. Benson Bana alipingana na mawazo ya Msigwa ambaye ni mbunge wa jimbo la Iringa Mjini.

Dk. Bana alieleza kuwa Mchungaji Msigwa anapaswa kufahamu kuwa kuna sababu za msingi zilizopelekea Rais asihudhurie sherehe hizo kwani ana washauri wengi wa masuala ya kidiplomasia.

“Hakuna mtu anayefahamu diary ya Rais au safari zake. Kwahiyo inasikitisha kuona mtu anamlaumu Rais kwa kutohudhuria ile sherehe bila kufahamu sababu zilizopelekea hilo,” Dk. Bana alieleza.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga alimuwakilisha Rais Magufuli na kusoma hotuba kwa niaba yake.

 

Utafiti: Farasi hubaini hisia za binadamu kwa kumuangalia
Fahamu Vyama vilivyosusia uchaguzi wa Marudio Zanzibar na vitakavyoshiriki