Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Masele Mipawa amemsimamisha kazi Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro iliyopo Arusha, Hezron Kyaruzi kwa kukosa uadilifu kwa mali za umma na kusababisha upotevu wa ng’ombe takribani 32.

Mlipwa ametangaza adhabu hiyo akiwa katika ziara ya kutembelea ranchi na kubainisha kuwa kutokana na matatizo mengi yaliyolikumba shamba hilo ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uongozi mbovu wa meneja hawana budi kumsimamisha kazi.

“Kutokana na upotevu wa ng’ombe, uzembe na ukosefu wa maadili tumeamua kumsimamisha kazi meneja wa ranchi na msaidizi wake na hatua nyingine za kisheria na kinidhamu zitafuata ” amesema Mipawa.

Ameongeza kuwa ziara aliyoifanya kwenye ranchi hiyo ni kwaajili ya ukaguzi kutokana na taarifa walizokuwa wakizipata ambazo zilionesha kuwa katika shamba hilo kumetokea upotevu wa ng’ombe ambao kampuni ya NARCO haina taarifa nao.

” Kati ya ng’ombe hao 32 waliopotea, 15 wameshapatikana na wengine 17 hawajapatikana mpaka sasa huku ng’ombe wengine 27 walichinjwa bila kibali cha makao makuu” ameongeza Mipawa.

Aidha amewaagiza wafanyakazi wengine waliobaki katika shamba hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, wazingatie nidhamu na uzalendo huku akiwaonya kuwa serikali haitavumilia mtu yeyote anayehujumu raslimali za taifa.

Hitimana: Bigirimana atawavaa Simba SC
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 22, 2020