Naibu Waziri wa Madini, Dkt.  Steven Kiruswa amesema biashara ya Makaa ya Mawe inatarajia kuleta tija kwa Watanzania, kutokana na uhitaji mkubwa wa madini hayo ndani na nje ya nchi, na kwamba wataendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa Makaa ya Mawe kutoka kwenye migodi

Dkt. Kiruswa, ameyasema hayo Novemba 12, 2022 Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma wakati alipotembelea mgodi wa uchimbaji wa Makaa ya Mawe ili kujionea shughuli za uchimbaji na kusema Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini ili kuvutia wawekezaji kufanya biashara ya madini mbalimbali yakiwemo Makaa ya Mawe.

Amesema,”Katika mikoa yote yanapochimbwa Makaa ya Mawe mnakaribishwa katika mkutano maalum utakaowasaidia kupata uelewa sahihi wa makaa ya mawe na madini mengine yanayopatikana katika mkoa huo na maeneo jirani.”

Mgodi wa makaa ya mawe.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo alisema, kutokana na uwepo wa migodi imesaidia wilaya hiyo kupata faida nyingi katika kutekeleza shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya na kusisitiza wadau wa Makaa ya Mawe katika Wilaya hiyo kushiriki mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Madini, ili kujifunza uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR).

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga amesema Makaa ya Mawe yanahitajika kwa wingi duniani kwa sasa na kuiomba Serikali itumie fursa hiyo kuhakikisha wilaya inapata faida ya uwepo wa migodi kwa kutoa ajira na kuleta maendeleo kwa jamii zinazozunguka migodi.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Ruvuma, Benedicto mshingwe amesema, hadi sasa wametoa ajira zaidi ya 700 kwa Watanzania hasa wanaozunguka mgodi na kubainisha kuwa wataendelea kushiriki katika shughuli za kijamii, ikiwemo ujenzi wa madarasa na zahanati.

Tahadhari yatolewa 'maambukizi' ugonjwa unaowatesa wengi
Waandamana kudai fidia mabadiliko tabianchi