Mwenyekiti  wa Bodi ya Taifa ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema amesema kuwa amepanga kuandaa mkakati utakaosaidia kuwapunguza magerezani wafungwa waliohukumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya ujambazi ambao watakubali kushirikiana kuwabaini wenzao.

Akizungumza jana ofisini kwake katika mahojiano maalum na E-FM, Mrema amesema kuwa atamuomba rais Magufuli kutumia mbinu aliyowahi kuitumia yeye kukomesha ujambazi nchini alipokuwa waziri wa mambo ya ndani, kwa kushirikiana na wafungwa hao ambao watakubali kuwafichua wenzao pamoja na kuonesha zilipo silaha walizokuwa wakizitumia.

“Nitaongea na wafungwa, wale ambao wamekubali kushirikiana na Serikali na kutorudia kufanya makosa, kama wale wa ujambazi. Nafanya kama walivyonisaidia zamani, kunionesha hizo silaha ziko wapi…bastola ziko wapi, mabomu yako wapi. Wakishanionesha mimi nitawapeleka kwa Rais nimuombe afute vifungo vyao au apunguze vifungo vyao,” alisema Mrema.

“Hata wale wa madawa ya kulevya, wale vijana ambao wako tayari kushirikiana na serikali ili tuwakamate wale mapapa walioko mitaani wanaoendelea kusambaza madawa,” aliongeza.

Aidha, Mrema alisema kuwa ataitumia Parole kuhakikisha anapunguza msongamano wa wafungwa magerezani kwa kuwabaini wale ambao wameonekana kujutia makosa yao na kuwa watii walikuwa magerezaji kisha kuwapa vifungo vya nje wakifanya kazi za kusaidia umma.

Amesema kuliko kuwarundika magerezani wakiongeza gharama, ni vyema zaidi wafungwa wenye sifa za kupewa kifungo cha nje wapewe kazi za kutumikia umma na kushiriki katika kuleta maendeleo.

Man Utd Waingia Kwenye Mtego Wa Juventus FC
Lowassa: Bavicha Twendeni Vijijini