Msajili msaidizi wa vyama vya Siasa nchini Sisty Nyahoza amesema uamuzi wa Kikao cha Halmashauri ya chama cha NCCR -Mageuzi wa kumsimamisha mwenyekiti wake James Mbatia na Sekretarieti yake yote kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho ni halali.

Nyahoza ameyasema hayo wakati akitoa uamuzi wa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa juu ya sakata hilo hii leo Mei 25, 2022 wa kumsimamisha Mbatia na wenzake hadi hapo itakapoamuliwa vingine kutokana na akidi ya wajumbe wa chama hicho.

“Kikao kilichofanyika Mei 21 mwaka huu kuwasimamisha Mwenyekiti (Mbatia) na sekretarieti yake kilikuwa ni halali na kwa mamlaka ya ofisi ya msajili inamtaka Mbatia kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi utakapotenguliwa,” amesisitiza Nyahoza.

Amesema baada ya tamko la kusimamishwa kwa viongozi hao Katibu wa chama cha NCCR -Mageuzi alipeleka barua kwa fomu ya kisheria ikijulisha kilichotokea katika chama hicho na kusema ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini imeridhia uamuzi huo.

“Sisi tumekubaliana na uamuzi huo kama Mbatia na wenzake hawataridhika ziko njia za kutafuta haki waende mahakamani,”amefafanua Nyahoza.

Mei 21 mwaka huu Mbatia na makamu Mwenyekiti Bara Angelina Mtahiwa walisimamishwa na Halmashauri Kuu ya NCCR kutojihusisha na shughuli za chama hadi watakapojieleza katika mkutano mkuu kutokana na tuhuma zinazowakabili ikiwemo ya kugombanisha viongozi.

Baada ya tukio hilo la Halmashauri Kuu Taifa ya NCCR-Mageuzi Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho ilikutana na kutoa maazimio manne ikiwepo kuwasimamisha nafasi za uongozi Makamu mwenyekiti Zanzibar Ambar Hamid, naibu Katibu Mkuu Zanzibar Amer Mshindan na mweka hazina Suzan Masele.

Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini la chama hicho Mohamed Tibanyendela amesema maazimio mengine ni kutotambua mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Mei 21 kutokana na kutokuwapo kwa mujibu wa Katiba na kuilaani Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia migogoro ya chama.

Akiongea katika kikao hicho Mbatia amesema NCCR – Mageuzi ni chama muasisi wa mageuzi nchini na wanaamini katika mwafaka wa kitaifa, huku akidai yaliyotokea ni changamoto za kawaida na wanaamini watazisimamia.

Uchinjaji Punda wasitishwa
Viongozi Young Africans wavamia kambi Shinyanga