Kuna mbinu nyingi za kushinikiza kupata kile unachoamini ni haki yako, lakini njia hii aliyoitumia mwalimu Hamisi Mumwi wa mjini Geita ni ya aina yake.

Duru kutoka Geita zinaeleza kuwa, mwalimu huyo aliyekuwa anafundisha shule ya msingi Mwagimagi mjini humo ameishi ndani ya darasa la shule hiyo akiwa na familia yake kwa kipindi cha miaka kumi sasa akidai stahiki zake baada ya kufukuzwa kazi kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi na baadae kumuoa.

Mwalimu huyo amewaeleza waandishi wa habari kuwa alifukuzwa kazi mwaka 2002 baada ya kushindwa kesi katika mahakama ya mwanzo lakini alikata rufaa katika mahakama ya wilaya na kushinda kesi hiyo. Anasema kuwa alirudishwa kazini lakini akafukuzwa tena mwaka 2005 kwa kosa lile lile alilolipangua mahakamani.

Ameeleza kuwa hatatoka katika darasa hilo hadi pale atakapolipwa stahiki zake na mwajiri wake ambaye ni serikali.

“Huyo alikuwa sio mwanafunzi kwa sababu alikuwa tayari amemaliza darasa la saba,” alisema mwalimu huyo na kusisitiza kuwa hatoki katika darasa hilo hadi atakapolipwa stahiki zake.

Hata hivyo, Afisa Utumishi wa Mji wa Geita, Lawrence Mhelela alieleza kuwa mwalimu huyo hana madai yoyote kwa serikali kwa sababu alifukuzwa kazi mwaka 2005 na kusafirishwa hadi nyumbani kwao Ukerewe kwa gari la serikali, lakini alirudi baadae na kuzusha madai hayo huku aking’ng’ania kuishi kwenye darasa hilo.

Alieleza kuwa mwalimu huyo ameonesha kuwa jeuri hivyo ataondolewa kwa nguvu katika darasa hilo na jeshi la polisi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Thomas Abraham alieleza kuwa kitendo cha mwalimu huyo kuishi darasani kimesababisha usumbufu kwa wanafunzi ambao wamelazimika kusoma kwa kupishana darasani.

“Darasa la tatu wanasomea nje ili kuwapisha darasa la kwanza na darasa la pili,” alisema Mwalimu Mkuu huyo.

Jumuiya ya Taasisi za Kiislam zapinga marudio ya uchaguzi Zanzibar
Utata: Ndege yapata ‘tobo’ kubwa angani