Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ujerumani Mesut Mustapher Ozil amerejea tena kwenye vyombo mbalimbali vya habari, akiongelea sakata lake la kugoma kupunguziwa mshahara kama sehemu ya kuendana na madhara ya mlipuko wa Corona duniani.

Ikumbukwe vilabu mbalimbali ulimwenguni vilipendekeza wachezaji wake kupunguziwa mishahara ili wawezekukidhi mahitaji ya kifedha za uendeshaji wa timu hizo. Arsenal ni moja ya timu iliyopendekeza na kutekeleza utaratibu huo.

Mengi yalizungumzwa kuhusiana na Ozil kugoma kupunguziwa mshahara wake lakini pia taarifa kutoka kwa Ozil mwenyewe hazikusikika sana.

Ozil amefunguka kuhusu sakata ilo na ameliongelea kwa ufupi sana akijilenga yeye mwenyewe na kile alichodai ni kulazimishwa kwa wachezaji kufanya maamuzi bila kushirikishwa ipasavyo.

Akizungumza na Athletics, Ozil amesema ” Kama wachezaji, tulitaka kuchangia. Lakini tulihitaji taarifa zaidi na tulikuwa na maswali mengi ambayo hayakujibiwa.”

“Ningekuwa tayari kuchukua hisa kubwa na pengine kukatwa mshahara kama ilipaswa kuwa hivyo mpaka pale mpira na hali ya kiuchumi ikiwa sawa. Lakini tulilazimishwa kufikia uamuzi huo  bila ya kuwa na majadiliano thabiti”.

“Kwa yeyote ambaye angekuwa kwenye hali hii, anahaki ya kujua kila kitu, kujua kinachofanyika na ni wapi pesa inakwenda.”

“Hatukupewa taarifa za kutosha, tulielekezwa kufanya maamuzi tu. Ilikuwa ni mapema mno kwa kitu ambacho kilikuwa ni muhimu na chenye msukumo mkubwa”

“Hii haikuwa sawa, hasa kwa wachezaji wadogo, na nilikataa. Nilipata mtoto na ninahudumia familia hapa Uturuki na Ujerumani na kwenye shughuli zangu za misaada. Nina mradi mpya wa kuwasaidia watu wa London, yale ni maamuzi yangu kutoka moyoni, sio kwa ajili ya kufurahisha watu.”

Ozil alitajwa kama mchezaji pekee wa Arsenal aliyekataa kupunguziwa mshahara katika kikosi cha Arsenal.

Katika hili, Ozil amesema “watu wanaonifahamu wananijua ni jinsi gani ninamoyo wa kusaidia wengine. Kwa kile ninachokijua. Mwisho wa siku, sio mimi peke yangu niliyekataa , ila ni jina langu pekee ndio lililotajwa.”

“Nafikiri ni kwasababu ni mimi, na watu wamekuwa wakitaka kunichafua kwa miaka miwili sasa. Wakitaka kunifanya nikose furaha, kuwasukuma mashabiki wanione mimi mbaya na kutengeneza picha ambayo sio sahihi.”

Ozil amecheza michezo yote tangu Arteta alipotua kunako Emirate. Lakini, tangu Ligi Kuu Uingereza – EPL kurejea, Ozil hajacheza mchezo wowote.

Ozil amesema, ” Labda maamuzi yangu yameleta madhara ndani ya uwanja, mimi sijui. Sitoogopa kusimamia kile ninachokiamini kuwa ni sawa, na kama mnakiona kinachotokea sasa hivi kwenye ajira, pengine nilikuwa sahihi.”

Juma lililyopita, Arsenal walitangaza azimio la kupunguza wafanyakazi 55 na inasemekana wachezaji wamekasirishwa na azimio hilo.

Ujerumani mambo magumu, Ligi Kuchezwa bila mashabiki
Msumbuji yapokea uenyekiti wa Baraza la mawaziri SADC