Jeshi la Polisi mkoa wa Singida limetangaza adhma ya kutafuta njia ya kumfungia mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kutumia mitandao ya kijamii kutokana na ujumbe uliosambazwa hivi karibuni kwenye mitandao ukionesha kuwa umeandikwa na mbunge huyo akiwa mikononi mwa Polisi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka amesema kuwa Jeshi hilo linawasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuona namna ya kuweza kumfungia Lissu kutumia mitandao ya kijamii kwa kufunga akaunti zake na makundi yote ambayo anashiriki.

Kamanda Thobias Sedoyeka

Kamanda Thobias Sedoyeka

“Tunaangalia uwezekano wa kushirikiana na TCRA, wamfungie kabisa katika ma-group ya mitandao ya kijamii,anakotumia kuandika lugha ya uchochezi na ya kuudhi dhidi ya serikali na uongozi uliopo,” alisema Kamanda Sedoyeka.

Kamanda huyo alisema kuwa endapo itabainika kuwa ujumbe ule ni wa Lissu kweli, Jeshi hilo litamfungulia mashtaka mkoani Singida ambako ndiko kosa hilo lilipotendeka. Alisema kuwa ujumbe ule ulijaa lugha za uchochezi zinazolenga kuwafanya wananchi kuichukia Serikali na iliyopo madarakani.

Wiki hii, Lissu alifanya mkutano wa hadhara jimboni kwake na kukamatwa muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake. Polisi walimsafirisha hadi jijini Dar es Salaam ambapo alihojiwa kwa saa kadhaa na baadae kulala rumande kabla ya kufikishwa mahakamani siku iliyofuata akisomewa mashtaka mawili ya uchochezi. Lissu alikana tuhuma hizo na Mahakama ilimuachia kwa dhamana hadi Agost 19 mwaka huu kesi hiyo itakapoitwa tena.

 

 

Makonda aandaa ‘matrekta’ kubomoa UKUTA wa Chadema
TRA yatangaza kukusanya kodi za nyumba za kupanga