Sakata la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza kupanda kwa bei ya umeme nchini limepelekea Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kuruguenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo na kumteua Dkt. Tito Esau kuchukua nafasi hiyo.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni saa chache baada ya Rais Magufuli kuwahakikishia wananchi kuwa hakutakuwa na ongezeko lolote la bei ya umeme. Rais Magufuli aliyasema hayo leo katika ibada ya Kanisa Katoliki, parokia ya Bukoba mkoani Kagera.

Rais Magufuli pia alimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa kuzuia uamuzi uliokuwa umetangazwa awali na Taneco na kuridhiwa na Ewura wa kupandisha bei ya umeme.

“Namshukuru Waziri wa Nishati ameshatengua maamuzi kwahiyo umeme hakuna kupanda, majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua,” alisema Rais Magufuli.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dkt. Tito Esau alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Lowassa: Trump ni mwamba asiyetabilika
Mambo 10 ya kufanya 2017 iwe ya mafanikio