Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezungumzia tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe anayeshikiliwa na jeshi la polisi.

Mbowe alikamatwa mkoani Mwanza alipokuwa akijiandaa kufanya kongamano la kudai Katiba Mpya. Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Mbowe alikamatwa baada ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yake za ugaidi na uhujumu uchumi kukamilika, na sasa ameshafikishwa Mahakamani. Tuhuma hizo hazina dhamana.

Akizungumzia sakata hilo wakati wa mahojiano maalum na BBC, Rais Samia amesema Mbowe alikuwa anakabiliwa na mashtaka hayo tangu Septemba mwaka jana, na kwamba polisi walikuwa wanaendelea na uchunguzi.

Alieleza kuwa wenzake ambao wanakabiliwa na mashtaka hayo kwa kushirikiana naye walishafikishwa mahakamani na wengine walihukumiwa.

“Ninavyojua Mbowe alifunguliwa kesi mwezi wa tisa mwaka jana, na kama ulivyosema mashtaka ni ugaidi nakuhujumu uchumi na wenzake. Nadhani wenzake kesi zao zimeshasikilizwa na wengine wameshapewa hukumu zao wanatumikia,” alisema Rais Samia.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi alifafanua jinsi ambavyo ‘anadhani’ Mbowe alicheza na mahesabu ili kuchanganya madai ya Katiba Mpya na kukamatwa kwake.  

“Yeye uchunguzi ulikuwa unaendelea. Tumekwenda tumeingia kwenye uchaguzi, tumemaliza uchaguzi… nadhani sasa Polisi wamemaliza uchunguzi wao wamemhitaji waendelee na kazi yao. Na kama utakumbuka, Mbowe kwa kipindi kirefu alikuwa Nairobi, sasa kwanini kakimbia, sijui. Lakini alipoingia tu nchini akaitisha maandamano ya Katiba Mpya. Nadhani ni mahesabu, akijua kwamba ana kesi ya aina hiyo, na hii vurugu ambayo anaianzisha akikamatwa aseme ni kwa sababu ya Katiba… nadhani, sina uhakika,” Rais aliiambia BBC.

Hata hivyo, Rais Samia aliongeza kuwa kwakuwa suala hilo liko Mahakamani, si vyema yeye kuendelea kulitolea maelezo zaidi.

“Nadhani tuache Mahakama zioneshe ulimwengu kwamba hizo tuhuma ni za kweli au sio za kweli, mahakama itaamua,” alisisitiza.

Hivi karibuni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro alisema kuwa kama kweli Mbowe anasali, awaambie wenzake ukweli kuhusu tuhuma zinazomkabili na kwamba hazina uhusiano wowote na masuala ya Katiba Mpya. Alisisitiza Kuwa Mbowe sio malaika, anaweza kufanya kosa kama mwananchi mwingine.

Kifaa kingine kimeshushwa Biashara United Mara
Ukonde aondolewa Young Africans