Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wananchi wote kila mmoja kwa nafasi yake kulinda afya yake kwani ulinzi wa afya unaanza na mtu mwenyewe.

Rais Samia ametoa rai hiyo Bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake wakati akielezea hali ya afya na hatua ambazo Tanzania imezichukua kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

“Kuhusu ugonjwa wa corona, kama mnavyofahamu, ugonjwa huu umeathiri dunia nzima na ubaya zaidi ni kwamba janga hili linapungua na kurudi katika mifumo tofauti tofauti”Mpaka sasa bado hakujawa na dalili za kupatikana kwa tiba ya maradhi haya. Njia pekee iliyopo ni kujikinga na kuchukua hatua mbali mbali za tahadhari,” amesema Rais Samia

“Hapa nchini tumekuwa tukifuata miongozo kadhaa ya kinga inayotolewa na wataalam, na kwa kutumia njia zetu za tiba asilia tumeweza kwa kiasi
kikubwa kushusha kiwango cha maambukizi”

“Hapa nchini, tumeamua kuunda Kamati ya Wataalamu ambao kwa kushirikiana na taasisi za Afya Duniani na zile za Kikanda za EAC na SADC wataliangalia suala hili kwa undani, kufanya uchambuzi wa kina na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua na jinsi ya kuendelea kupambana na maradhi hayo”

“Hivyo, wakati tukisubiri majibu ya Kamati iliyoundwa, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari zote kama zinavyoshauriwa na wataalam. Nawaomba kila mmoja awajibike kwani ulinzi wa afya yako unaanza na wewe mwenyewe,” amesema Rais Samia.

Rais wa Chad kuzikwa leo
TMA yatahadharisha Kimbunga Jobo kupiga Tanzania