Uongozi wa klabu ya Stand United, uliochaguliwa kwa kukosa baraka za shirikisho la soka nchini TFF, jana ulikutana na waandishi wa habari mjini Shinyanga na kuitangaza kuwaacha wachezaji saba kutokana baadhi yao kumaliza mkataba wao na wengine kujisajili na timu za nje.

Akitangaza uamuzi wa timu kwa waandishi wa habari katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga, Dkt. Ellyson Maeja aliyejitambulisha kama mwenyekiti aliyechaguliwa kupitia uchaguzi wa mwishoni mwa juma lililopita, alisema uamuzi huo ulifikiwa siku ya jumatatu baada ya kikao cha kamati ya utendaji cha timu hiyo kuketi na kujadili mambo kadhaa ya kuijenga klabu hiyo.

Dkt. Maeja aliwataja wachezaji walioachwa kuwa ni Haruna Chanongo, Abuu Ubwa, Nasoro Masoud Chollo, Hassan Seif Banda na Philip Methusela.

Kwa upande wa wachezaji waliomaliza mikataba yao, aliwataja kuwa Salum Kamana na Elias Magul ambao alidai kuanzia sasa wako huru kujiunga na klabu yoyote na kuongeza kuwa wachezaji wengine wa timu hiyo wataendelea kuichezea Stand United msimu ujao.

Dkt. Maeja alisema kikao cha kamati ya utendaji kimeridhia kuwa Kenedy Nyangi kuwa katibu mkuu wa muda wa Stand United na Emmanuel Kaombwe kuwa katibu msaidizi mpaka pale atakapopatikana katibu kulingana na katiba ya klabu hiyo.

Mwenyekiti huyo wa Stand United aliongeza kuwa, kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo mwenyekiti ana mamlaka ya kuteua wajumbe wawili wa kamati ya utendaji na kwamba tayari ameteua mmoja ambaye ni Sudy Rashid na nafasi nyingine iliyobaki ataitangaza baadae.

Katika hatua nyingine Dkt. Maeja alisema kikao hicho cha kamati ya utendaji kimeunda kamati ya ufundi na usajili na kumtangaza bwana Geofrey Tibakyenda kuwa mwenyekiti wa wa kamati hiyo.

Mwenyekiti wa Acacia Stand United, Dr. Maeja alisema tayari uongozi wa Stand United umeanza kazi na orodha ya wachezaji wa timu hiyo na makocha wapya kutoka nje ya nchi watatangazwa siku chache zijazo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Geofrey Tibakyenda aliwataja wajumbe wa kamati ya ufundi na usajili kuwa ni Richard Abwao,Meja Mohammed Ndalo,Mbasha Matitu,Mwalimu Gasper Coach na Sudy Rashid.

Tibakyenda alisema kamati yake itakamilisha usajili wake wiki chache zijazo na kocha msaidizi kutoka nchini Ufaransa Denis Guillume atakuwepo wakati wa usajili huo akishirikiana na kocha mkuu Patrick Leweg.

Viongozi hao wamewataka wananchi na wadau wa michezo mkoani Shinyanga kujitokeza kushirikiana na uongozi huo mpya ili timu hiyo iweze kufanya vyema msimu ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Viongozi wapya wa Stand United waliochaguliwa mwishoni mwa juma lililopita ni Dkt. Ellyson Maeja aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa timu hiyo huku Richard Luhende akichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni Francisco Magoti, Geofrey Tibakyenda ,Jackline Burahi,Twahil Njoki na Mariam Richard.

Hata hivyo shirikisho la soka nchini TFF, lilitangaza kusimamisha zoezi la uchaguzi wa klabu ya Stand Utd, kufutia kuibuka kwa mvutano wa pande mbili ambazo zote zilikua zinaendesha harakati za kutaka kufanya uchaguzi.

Uongozi wa Stand Utd kampuni unaoongoza na Aman Vicent, umekua ukipigwavita na baadhi ya wadau wa soka mkoani Shinyanga wanaojiita Stand Utd wanachama, halia mbayo iliibua mtafaruku mkubwa na kutoa msukumo kwa TFF kufanya maamuzi ya kusimamisha zoezi la uchaguzi.

Nchi iko salama - Serikali
Pablo Zabaleta Asaka Njia Ya Kumuepuka Guardiola