Hifadhi ya taifa Tanzania (TANAPA), imethibitisha kutokea kwa kifo cha Mnyama wa porini Simba maarufu kama ‘Bob Junior’ aliyeishi katika hifadhi ya Serengeti baada ya kushambuliwa na kundi la Simba watatu waliokuwa na lengo la kuuangusha utawala wake.

Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi hiyo, Fredy Shirima amesema tukio hilo ni asilia katika uhifadhi lakini pia hutokea zaidi kwa Simba ambao hushikilia ngome dhidi ya wengine wanaoitaka ngome.

Amesema, “Bob Junior aliuawa siku ya Machi 11, 2023 katika shambulizi la Simba watatu ambao walikuwa sehemu ya kundi la simba saba waliokuwa wanapanga mapinduzi.

“kwa kawaida hatuwezi kuingilia maisha ya wanyama pori… hivyo kilichotokea kilipangwa miongoni mwao ikiwa ni vita vya kimapinduzi na simba huwa wana tabia hiyo ambapo mtawala anapozeeka hutolewa kimabavu,” alieleza.

Shirima anasema, ‘Bob Junior’ pia alikuwa na sifa za kipekee kama vile kuwa na manyoya mengi zaidi kuliko simba wengine lakini mwenye kuvutia kwa muonekano na hutulia pale anapopigwa picha.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, ni Simba huyo aliyejibebea umaarufu kwa kuwa mpole na anayekuwa na utulivu anapoona watalii.

Kufuatia tukio hilo, Wadau wa utalii wamesikitishwa na kifo cha simba huyo, huku ikimtaja kuwa ndiye Simba bora na mtulivu kuwahi kuonekana katika hifadhi ya Serengeti.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Tanzania ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya simba kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika ambapo inakadiriwa kuwa na simba 15,000 huku hifadhi ya Serengeti pekee ikiwa na takribani simba 3,000.

Meneja Arsenal amtahadharisha Gabriel Jesus
Gerson Msigwa: Sipendezwi na sakata la Fei Toto