Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, ni moja ya kampuni za madini zinazoongoza nchini kwa kutafsiri na kutekeleza vyema matakwa ya Sheria ya Madini iliyofanyiwa maboresho mwaka 2017, huku ikiinufaisha jamii inayozunguka mgodi, kuupa sifa Mkoa wa Geita na wizara ya madini.

Dkt. Kiruswa ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea banda la GGML katika maonesho ya Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jijini Arusha lililozikutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma wa madini kwenye migodi ya madini na taasisi za kifedha.

Amesema GGML imetekeleza vyema matakwa ya sheria hiyo katika utoaji wa huduma kwenye jamii unaofanywa na migodi ya madini (CSR), ambapo Mwanasheria Mkuu wa GGML, David Nzaligo alisema kila mwaka kampuni hiyo hutenga zaidi ya Shilingi bilioni tisa, zinazotekeleza miradi mbalimbali ya kijamii chini ya usimamizi wa Halmshauri na Wilaya za Mkoa wa Geita.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stephen Kiruswa, akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) alipotembelea banda la kampuni hiyo katika maonesho ya Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jiji Arusha. (Kushoto) ni Wakili Mwandamizi wa Sheria wa GGML, David Nzaligo na wengine ni maofisa waandamizi kutoka Madini.

Hata hivyo, Dkt. Kiruswa alisema mafanikio ya maboresho ya sheria ya madini yaliyopelekea kutungwa kwa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini, yalichochea ongezeko la fursa mbalimbali katika nafasi za ajira na mafunzo, uhaulishaji wa teknolojia, utafiti na maendeleo, matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa na watanzania.

Akizungumzia mfumo wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini (Local Content), Dk. Kiruswa amesema mfumo utawezesha kampuni za uchimbaji wa madini na watoa huduma kwenye migodi ya madini kuwasilisha nyaraka mbalimbali kwenye mfumo huo kwa njia ya kieletroniki badala ya kutumia nakala ngumu kama ilivyokuwa ikifanyika awali.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stephen Kiruswa akipokea zawadi kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Stephen Mhando (kulia) alipotembelea banda la kampuni hiyo katika maonesho ya Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jiji Arusha. Kushoto ni maofisa waandamizi kutoka Madini.

GGML, katika utekelezaji wa mfumo huo, imetoa zabuni kwa kampuni za ndani katika utoaji wa huduma mbalimbali ikiwamo usafirishaji kwa kampuni ya Blue Coast ambayo inamilikiwa na mtanzania na Dk. Kiruswa amefafanua kuwa watanzania katika migodi mikubwa zimeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi kufikia 15,341 mwaka 2022.

Kwa upande wa GGML imeajiri zaidi ya wafanyakazi 2,249 na wakandarasi 4,152 asilimia 97 ni raia wa Tanzania na sheria hiyo imesaidia kuongeza manunuzi ya ndani kwa mwaka 2022 jumla ya Dola bilioni 2.22 sawa na asilimia 97.4 ya manunuzi yote ya kampuni za madini yalifanyika kwa kutumia kampuni za watanzania, ukilinganisha na Dola milioni 238.71 sawa na asilimia 46 ya manunuzi yote kwa mwaka 2018 kutumika.

Serikali yataka kipaumbele huduma Watoto wenye ulemavu
Bondia Fadhili Chamile mikononi mwa Polisi Dar