Muimbaji nguli wa Uingereza, George Michael amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 53.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na muwakilishi wake aliyeeleza kuwa, “kwa masikitiko makubwa tunathibitisha kifo cha mwanetu mpendwa, kaka na rafiki George aliyetutoka kwa amani akiwa nyumbani kwake katika kipindi hiki cha Christmas.”

Chanzo cha karibu cha mwimbaji huyo kinachoaminika kimeiambia TMZ kuwa alifariki kutokana na moyo kushindwa kufanya kazi wakati akiendelea kurekodi kipande cha filamu kilichopaswa kurushwa kwenye kituo kimoja cha runinga nchini humo mwezi Machi.

George atakumbukwa kwa nyimbo zake kubwa zisizochuja masikioni mwa mashabiki wa muziki mzuri ukiwemo wimbo wa ‘Careless Whisper’, ‘Wake me Up Before You Go-Go,’ ‘Last Christmas’ na ‘Freedom’.

Alianza kufahamika kwenye ulimwengu wa muziki mwaka 1982 akiwa na kundi la ‘Wham!’ baadae akajiunga na ‘Band Aid’.

Alifanikiwa kuuza nakala zaidi ya milioni 100 kupitia aina yake ya muziki iliyobatizwa jina la ‘post-disco dance-pop’.

Apumzike kwa Amani!

Manara amuombea msamaha Jerry Muro
Ronaldo avishwa taji la ‘mfalme’ wa mitandao ya kijamii 2016