Mlinzi wa kati wa Mbeya City  Fc, Tumba Sued Lui, huenda akaukosa mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya Tanzania Prison uliopangwa kuchezwa jumamosi hii kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Kwenye mazoezi asubuhi ya leo,Tumba amepatwa na jeraha kubwa kwenye paji la uso lililomfanya kushonwa nyuzi tatu hapo hapo baada ya kugogwa kiwiko (kwa bahati mbaya) na nahodha Temi Felix walipokuwa wakiwania mpira.

Mkuu wa kitengo cha utabibu kwenye kikosini Dr Joshua Kaseko, amesema atatoa taarifa ya mwisho siku ya kesho kama mlinzi huyo atakuwa mmoja wa nyota watakaowakilisha City kwenye mchezo huo wa jumamosi.

“Tumemshona nyuzi tatu, taarifa ya yeye kucheza mchezo wa jumamosi nitaitoa kesho,hii ni kwa sababu nataka  kutizama maendeleo yake ndani ya saa 24 zijazo,tukio hili limemsikitisha kila mtu lakini kwenye soka mambo haya hutokea, mimi pamoja na wenzangu(kitengo cha utabibu)  tutajitahidi kuhakikisha anakuwa sawa tayari kwa mchezo huo  kwa sababu mwalimu (Phiri) ameniambia kuwa anamuhitaji kama mtu muhimu kwenye safu ya ulinzi”, alisema. 

Akiendelea zaidi  Dr Kaseko amesema kuwa mlinzi wa kati Deo Julius  aliyeumia kwenye  mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara  dhidi  Tanzania Prison wiki mbili zilizopita anatarajia kuanza mazoezi jumatatu hii kufuatia kupona  kwa majereha  ya goti aliyokuwa ameyapata.

“Deo Julius  sasa yuko tayari,  ni uhakika kuwa ataanza mazoezi jumatatu, amekuwa nje kwa wiki mbili tukimuunguza majeraha ya goti, hili ni jambo jema kwetu kwa sababu  kurejea kwake kikosini kunakuja kuimarisha safu yetu ya  ulinzi  alisema” Dr Kaseko.

Chanzo: mbeyacityfc

Sexwale Ajiondoa Uchaguzi Wa FIFA
Nadir Haroub: Nimefurahishwa Na Hatua Ya Kurudi Kwangu