Vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, jana vilitoa tamko lao rasmi kupinga kauli ya Rais John Magufuli kuwataka wanasiasa na wananchi kuacha siasa hadi baada ya miaka mitano watakapokutana kwenye Uchaguzi Mkuu bali sasa wafanye kazi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti ya uchaguzi wa mwaka 2015 na Tume ya Uchaguzi, Rais Magufuli aliwataka watanzania kujikita katika kufanya kazi na kwamba siasa zifanywe ndani ya Mabaraza ya Madiwani na Bungeni kwa waliochaguliwa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amepinga kauli hiyo akimtaka Rais Magufuli kukumbuka kuwa siasa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na ni mfumo unaogusa maisha ya kila siku. Alisema katika mfumo wa uongozi wapo watu ambao wameajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi ya siasa na ni kazi halali kikatiba.

“Rais Magufuli anatakiwa kujua siasa siyo starehe, bali ni kazi kama zilivyo nyingine zozote. Uhalali wa kazi za siasa unatolewa na Katiba aliyoapa kuilinda na kukaziwa na Sheria Namba 5 ya mwaka 1992 (Political Parties Act NO. 5 of 1992) pamoja na marekebisho yake,” alisema Mbowe.

Alisema kwakuwa kuendesha siasa kwa kufanya mikutano, makongamano na maandamano ni haki iliyotambulika kisheria na katika Katiba ambayo Rais ameapa kuilinda, Ukawa wataendelea kufanya mikutano bila kujali agizo hilo huku akiitaka Serikali kuandaa magereza za kutosha endapo watataka kuwafunga.

“Aandae magereza ya kutosha kwa sababu hatutazibwa midomo… kama wananchi wananyimwa fursa ya kusema ni vibaya, watatumia vitendo mambo ambayo yalileta vita katika nchi za wenzetu,” alisema.

Aliwataka washauri wa Rais kumshauri kutengua kauli hiyo kwani hawataacha kufanya mikutano ya kisiasa na shunghuli nyingine za kisiasa hata wakiwa nje ya Bunge. Alisema Serikali imewaziba midomo bungeni na sasa inataka wasifanya siasa nje ya Bunge na wao hawako tayari kukubaliana na hilo.

Kauli ya Mbowe iliungwa mkono na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia ambaye alisema kuwa hawaiombi Serikali ruhusa ya kufanya siasa kwani ni haki yao kikatiba.

Ukawa wameazimia kukutana hivi karibuni ili kujadili hatua hizo na kutoa tamko la pamoja juu ya hatua walizopanga kuchukua.

Msajili wa vyama vya Siasa aitetea kauli ya Magufuli kuhusu Siasa
Majina ya Waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha 5 haya hapa