Upinzani sio kupinga kila kitu, hicho ndicho kinachoanza kuonekana kwa baadhi ya Wabunge wa chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema.

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka ambaye ni mbunge wa jimbo la Same Mashariki kwa tiketi ya Chadema, amejitokeza kusifia na kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kuziba mianya ya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kupitia mishahara hewa.

Kaboyoka amesema kuwa anaunga mkono pia jitihada za rais Magufuli kupunguza mishahara ya vigogo katika taasisi za umma.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kuwa atapunguza mishahara ya baadhi ya watumishi wanaopata hadi shilingi milioni 40 kama mshahara, na kuwashusha hadi kiwango cha milioni 15.

Mbunge huyo kada wa Chadema alimshauri rais Magufuli kutumia fedha hizo katika kuboresha sekta za Afya na Elimu nchini kwa maslahi ya wananchi ambao wengi ni maskini.

“Naunga mkono sana hatua za Rais, kuna sababu gani mfano watumishi wa umma kulipwa wastani wa hadi shilingi milioni 20?” alihoji.

“Mifano mingine Rais ameitaja, anahitaji kuungwa mkono ili huduma za kijamii ziboreshwe,” aliongeza Kaboyoka.

Mwishoni mwa mwaka jana, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi pia alionesha kukubali kasi ya Rais Magufuli aliyoanza nayo na kuwataka madiwani wa jimbo lake kuhakikisha wanaendana na kasi hiyo ili kutowapa watu nafasi ya kutamani Halmashauri ya jiji hilo kutawaliwa na CCM.

Makonda awapa Mrisho Mpoto, Banana Zorro dili ya usafi
Mapenzi: Mrembo alipia Bango katikati ya jiji akitangaza kuwa bikira, adai anasaka ‘tendo’ kabla hajafa