Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, ametoa siku saba kwa wakazi wa Msalato waliojiorodhesha kudai fidia ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato kwa njia ya udanganyifu, kufika ofisi za serikali ya mtaa kuondoa majina hayo kwa hiari.

Mtaka ametoa agizo hilo Julai 22, 2022, wakati akizungumza na maafisa ardhi na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kwenye mkutano kuhusu wimbi lililoibuka la wananchi kuvamia maeneo ya Serikali.

Amesema, watu wanaibuka na kutwaa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya Kitaifa ikiwemo barabara ya mzunguko (ringroad) na uwanja wa Ndege wa Msalato kwa lengo la kudai fidia kinyume cha sheria.

Uwanja wa ndege Dodoma.

“Kwa watakaotoa majina yao ndani ya siku saba wataruhusiwa kufanya hivyo bila kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria na kwa watakaokaidi agizo hili timu itafanya msako mkali kubaini wanaodanganya kuhusu zoezi hilo,” amesema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema kwa watakaobainika kufanya ukaidi huo watahukumiwa kifungo cha miaka saba jela.

Hata hivyo amesema wakazi waliojenga kwenye hifadhi ya barabara ya mzunguko waondoe nyumba zao na maendelezo yoyote yaliyopo na atakayekaidi agizo hilo Serikali itabomoa nyumba zao na watalipa gharama za ubomoaji huo.

Utamaduni wa Mtanzania wapigiwa vigelegele na Serikali
Rais Samia akemea uharibifu wa barabara