Wakulima Wilayani Mbulu wameiomba serikali iwapelekee wataalamu wa kilimo na pembejeo za kutosha ili kuwawezesha kuwa na kilimo chenye tija zaidi.

Ombi hilo limetolewa na umoja wa Wamwagiliaji wa Skimu ya umwagiliaji ya Mangisa iliyopo katika kata ya Dongobeshi, Wilayani Mbulu Mkoani Manyara walipokuwa wakizungumza na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji walipoitembelea Skimu hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya umoja wa wakulima wa umwagiliaji, katibu wa umoja huo, Damiano Sulle amesema kuwa serikali kwa kushirikiana na wafadhili ilifanya jambo la msingi kupeleka Skimu ya umwagiliaji katika eneo hilo ambapo ameeleza kuwa imeleta tija kwani ndio ajira pekee iliyo badilisha maisha ya wakazi wengi katika kata ya Dongobeshi.

“Kabla ya kuwepo kwa Skimu hii mkulima aliweza kuvuna chini ya gunia kumi (10) au kumi na tano (15) za Vitunguu saumu kwa hekta na baada ya kuboreshwa kwa miundombiu ya kisasa ya umwagiliaji mkulima anaweza kupata hata gunia hamsini (50) ya zao hilo kwa hekta”, amesema Sulle.

Aidha, ameiomba serikali kuwasaidia kusakafia mfereji ambao haujasakafiwa wenye urefu wa mita 50 ambao utawasaidia wakulima kujipanga vizuri hasa katika matumizi sahihi ya maji na kuongeza uzalishaji zaidi wa mazao.

Sambamba na hilo wakulima wameomba serikali kuwatafutia soko la uhakika hususani la zao la kitunguu swaumu ili waweze kuuza zao hilo kwa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani kwani wana maghala makubwa ya kutosha ambapo wangeweza kuhifadhi mazao hayo na kuyauza wakati ambao bei za mazao hayo zikiwa juu.

Hata hivyo, Wilaya hiyo ya Mbulu ina eneo la Hekta 2400 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na hekta 1250 ndizo zinazotumika kwa kilimo hicho ambapo kuna Skimu saba ambazo ni Mangisa, Dongobeshi, Tumati, Diyomati, Dirm, Ari na Bashay skimu ambazo zinatumika kwa kilimo cha zao la mahindi, Viazi, Shayiri na mazao mengine ya mbogamboga.

Video: Ni lazima kuwe na nidhamu kwenye matumizi ya bajeti- Prof. Lipumba
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 17, 2019