Sakata la kupandishwa kwa bei ya umeme lililopelekea kuondolewa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba limegharimu wakurugenzi wengine wa shirika hilo.

Taarifa kutoka katika shirika hilo zimeeleza kuwa Wakurungezi watatu wa shirika hilo wameshushwa vyeo na kuhamishiwa katika chuo cha Tanesco (TSS) kilichoko jijini Dar es Salaam.

Vigogo hao waliotajwa kutumbuliwa vyeo vyao ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Usambazaji na Huduma kwa Wateja, Mhandisi Sophia Mgonja, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mtendaji (Usafirishaji), Mhandisi Declan Mhaiki na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji), Nazir Kachwamba.

Aidha, Mhandisi Khalid James, mratibu wa mradi wa ujenzi wa njia mpya ya umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga aliyedaiwa kuwa ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji) alikanusha kupata taarifa za uteuzi wowote jana.

Chanzo cha uhakika cha gazeti la Mwananchi kilieleza kuwa uamuzi wa mabadiliko hayo ulifanyika kupitia kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Justine Ntalikwa alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema, “hayo yanawahusu Tanesco, mpigieni msemaji wake anaweza kukupa ushirikiano.”

Msemaji wa Tanesco alipotafutwa jana kwa njia ya simu hakupatikana na hata alipotumiwa ujumbe hakuweza kujibu.

Chanzo: Mwananchi

Kanisa lamuombea Rais Magufuli
Majaliwa aonya ujenzi holela Kigamboni