Baadhi ya wananchi wameikosoa vikali Clouds TV kupitia kipindi chake cha ‘Take One’ kinachoongozwa na Zamaradi Mketema, kwa kumualika mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja (shoga) na kufanya naye mahojiano, Jumanne, Juni 28 mwaka huu.

Watumiaji hao wa mitandao  ya kijamii wamedai kuwa kituo hicho kilienda kinyume na maadili ya vyombo vya habari pamoja na kanuni zake na kuitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuichukulia hatua kali kwa mujibu wa taratibu za urushaji matangazo.

Clouds malalamiko

Hatua hiyo iliwapelekea kituo hicho kumfanyia mahojiano Zamaradi Mketema kupitia kipindi cha 360 ili kusafisha hewa na kueleza sababu zilizopelekea kufanya kipindi hicho kwa mlengo huo.

Mtangazaji huyo alieleza kuwa waliamua kufanya hivyo kwa lengo jema kwani tatizo hilo ni kubwa katika jamii na liko wazi hivyo walitaka jamii ifahamu kinachoendelea na kuchukua hatua stahiki ya kutatua.

“Tusisubiri mambo yaharibike zaidi ndio tuanze kuzungumza lazima tuchukuwe hatua sasa, kama tunavyoweza kumhoji mwathirika wa madawa ya kulevya na kuamini kwa kujua njia alizopitia tutaweza kuepuka na kuwaelimisha ndugu na jamaa zetu ndivyo hivyo tujifunze walipokosea hawa,” Zamaradi anakaririwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikuwa mmoja kati ya waliopiga simu kueleza mtazamo wake kuhusu hatua hiyo ambapo alikitetea kituo hicho na kueleza kuwa kilichofanya ni sahihi kwani kimeweka wazi tatizo kwa mlengo chanya kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi.

“Tuamke na hizi hasira tuelekeze kwenye tatizo ambalo lipo kwenye jamii yetu, wazazi na walezi tujenge tabia ya kukagua watoto wetu tukiamka pia majirani zetu. Sisi kama Serikali tumeamshwa na pia inabidi waanze kutaja wateja wao ili jamii iwafahamu kwani inawezekana wateja wao wengine ni viongozi wa serikali,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

TCRA imekuwa na kitengo maalum cha kupokea malalamiko ya wananchi na watumiaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano hivyo inatarajiwa kulitolea ufafanuzi suala hilo.

Mahakama Kuu Arusha Yatengua Ubunge wa Onesmo Nangole
Utumbuaji majipu watua Zanzibar, vigogo 12 watupwa nje