Kampuni ya ndege ya Fastjet imewawapandisha vyeo marubani wawili raia wa Tanzania waliotajwa kwa jina la Abeid na Soud kuwa Marubani wakuu wa shirika hilo.

Kwa mujibu wa Fastjet, Abeid na Soud ambao walianza kazi katika shirika hilo mwaka 2014 kama marubani wasaidizi, wanakamilisha idadi ya marubani 10 Watanzania wanaofanya kazi katika shirika hilo la ndege linaloongoza kwa viwango nafuu vya nauli nchini na kutoa huduma bora zaidi.

Akizungumzia jinsi alivyojiunga na urubani, Abeid alisema kuwa ilikuwa ndoto yake tangu akiwa mtoto na alivutiwa kufanya kazi hiyo kupitia baba yake ambaye alikuwa ni mhandisi wa ndege.

Alisema kuwa baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alipata fursa ya kusomea mafunzo ya ndege, Port Elizabeth nchini Afrika ya Kusini baada ya kupata udhamini wa mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TCAA).

Haikuwa tofauti sana kwa Soud ambaye alitamani sana kuwa rubani ingawa alikutana na changamoto za kifedha. Soud alifanikiwa kuingia katika masomo ya urubani Asia Pacific Flight training kwa muda wa miaka miwili, baada ya kumaliza Chuo kikuu. Alihitimu mafunzo ya urubani mwaka 2009 na kisha alirudi nyumbani ambapo alianza rasmi kufanya kazi ya urubani.

“Marubani hawa wa kitanzania wanafurahia kufanya kazi kwenye shirika la bei nafuu la Fastjet kwasababu wameweza kuwasafirisha abiria wengi ambao ni wasafiri wa mara ya kwanza na hivyo wanajihisi kuwa ni sehemu ya mabadiliko na ukuaji uchumi kwa nchi yetu. Hii ni kwa sababu hivi sasa watu wengi zaidi wanaweza kutumia usafiri wa anga na kufika kwenye biashara zao kwa wakati,” Afisa Mahusiano na Masoko wa shirika hilo, Lucy Mbogoro aliiambia Dar24.

Aliongeza kuwa shirika hilo linaajiri marubani wa Kitanzania kila mwaka ili kuchangia ukuaji wa ajira kwa wazawa.

“Marubani hawa pia wanashauri vijana kufuata ndoto zao kwasababu fursa za ajira katika sekta ya anga zipo na sekta hii inakuwa kwa kasi sana hivyo wasiachie fursa hizi,” alisema Mbogoro.

Video: Mazuu ampa shavu zito msanii wa Kenya, waachia video hii
Serikali Kuanza Kutoa Hati Miliki Na Upangaji Miji