Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Jumatano, 14 Septemba, 2016) amezindua miongozo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi  na kuziagiza taasisi za umma na binafsi zianze kutumia mfumo huo ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.

Majaliwa amezindua miongozo hiyo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni mjini Dodoma ambapo amewaagiza BRELA (Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara) kuhakikisha wanajumuisha anauani za makazi kwa waombaji wa leseni za biashara ili kurahisisha utambuzi na uhakiki.

Amesema mfumo huo lazima uweke msukumo mpya wa kimkakati ili kuhakikisha uwekaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi na Postikodi unatekelezwa ipasavyo na unachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, na unatakiwa ukamilike nchi nzima kabla ama ifikapo Juni, 2018 ila kasi ya utekelezaji wake inakwamishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa fedha na barabara au mitaa mingi kutokuwa na majina.

Majaliwa amewataka wadau wote kutimiza wajibu wao katika utekelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kulingana na maelekezo yaliyo kwenye miongozo hiyo, huku akieleza kuwa Serikali ya awamu ya tano inapenda watendaji wake kuwa wabunifu, hivyo changamoto hizo zitatuliwe haraka na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Waziri Mkuu pia ameziagiza Halmashauri zote nchini kuzitafutia ufumbuzi changamoto ambazo hazihitaji fedha ama gharama kubwa kama kuhakikisha barabara na mitaa yote inakuwa na majina yaliyorasimishwa na kudhibiti mipango miji dhaifu na ujenzi holela.

Hivyo, amezitaka Halmashauri kuwa na takwimu za idadi ya barabara na mitaa na nyumba katika kila kata na kuwa na taarifa za wakazi wa kila kata, kujenga uelewa na uwezo wa mfumo kwa wadau na wananchi na kuimarisha matumizi ya daftari la wakazi.

Serikali Yashauliwa Kutumia Wataalamu Wa Jiolojia Katika Shughuli Za Ujenzi
UEFA Wapata Rais Mpya, Kuongoza Hadi 2019