Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania ulifanyika jana na kukishuhudia mwanariadha wa zamani, Wilhelm Gidabuday akirithi mikoba ya Katibu Mkuu wa zamani Suleiman Nyambui aliyeko nchini Brunei.

Nyambui kwa sasa ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha ya Brunei.

Aidha katika uchaguzi huo Anthony Mtaka aliitetea nafasi yake ya Urais wa shirikisho hilo kwa mara nyingine tena kwa kura 73 kati ya kura 74.

Gidabuday alipata kura 38 akiwapita Michael Washa (24) na Gidamis Shahanga (11) huku kura moja ikiharibika katika nafasi hiyo.

Katika nafasi nyingine, William Kalaghe alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Utawala kwa kura 59 dhidi ya 15 zilizokwenda kwa Zainab Mbilo huku Dk. Ahmed Ndee alichukua nafasi ya Makamu wa Rais Ufundi kwa kura 74 dhidi ya kura nne za hapana.

Ombeni Zavalla aliyekuwa akikaimu Katibu Mkuu wa RT katika uchaguzi huo alipita bila kupingwa katika nafasi ya Katibu Mkuu Msaidizi kwa kura zote 74 na Gabriel Liginyani akipata nafasi ya Mweka  Hazina wa shirikisho hilo kwa kura 69 kati ya 74.

Wengine waliopata nafasi ya Ujumbe wa RT ni Lwiza John, Meta Petro, Robert Kalyahe, Dk. Nassoro Matuzya, Rehema Killo, Zakaria Barie, Mwinga Mwanjala, Tullo Chambo, Christian Matembo na Yohana Misese.

Dani Alves: Nipo Salama, Sikuvunjika
Mzimu Wa Majeraha Wamuandama Mathieu Debuchy