Kikosi cha Mabingwa wa Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 Young Africans, kitarejea mazoezini Jumatatu (Januari 25) kuanza maandalizi ya mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC).

Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans Haji Mfikirwa amesema wachezai wote wakiwemo waliosajiliwa wakati wa dirisha dogo la usajili Dickson Job na Fiston Abdul Razak, wataripoti kambini Kigamboni siku hiyo.

“Tunatarajia kuanza kambi Januari 25, itakua siku ya Jumatatu ya wiki ijayo, wachezaji wote waliokua Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi sambamba na wale tuliowasajili wakati wa dirisha dogo, watajumuika kwa pamoja, ili kuanza maandalizi.”

“Tunaamini muda watakaokaa kambini hadi ligi itakaporejea watakua wamepata kitu kutoka kwa kocha Cedric Kaze pamoja na wenzake wanaounda benchi la ufundi, dhumuni letu msimu huu ni kurejesha heshima ya ubingwa wa Tanzania Bara iliyopotea kwa misimu mitatu iliyopita.” Amesema Mfikirwa

Baada ya kurejea kutoka Zanzibar, kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Kocha Mkuu wa Young Africans Cedric Kaze aliwapa wachezaji wake mapumziko ya siku kumi, na muda huo utakamilika Januari 25.

Young Africans wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa wamejikusanyia alama 44 baada ya kushuka dimbani mara 18, wakishinda michezo 13, wakitoka sare michezo 5 huku wakisalia kuwa timu pekee ambayo haijafungwa kwenye ligi hiyo.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 21, 2021
Kasi ya saratani yaongezeka nchini