Mshambuliaji wa Brazil, Neymar amesema angependa kucheza tena na Lionel Messi wa Inter Miami katika siku zijazo.

Wawili hao ni marafiki wazuri na walicheza pamoja kule Barcelona na Paris Saint-Germain, lakini hawatamenyana katika michuano ya Copa America majira ya joto baada ya mchezaji huyo wa Kimataifa wa Brazil kupata jeraha la goti Oktoba mwaka jana.

Tangu ilipomsajili Messi katika majira ya joto ya 2023, Miami imewaongeza wachezaji wenzake wa zamani wa Barcelona, Sergio Busquets, Jordi Alba na Luis Suarez kwenye kikosi hicho.

Alipoulizwa kuhusu Messi kuwaleta marafiki zake Inter Miami na kama angependa kucheza naye tena, Neymar aliiambia ESPN Argentina: “Natumai tunaweza kucheza pamoja tena.

“Leo ni mtu mzuri, kila mtu anamfahamu katika soka na nadhani ni mzuri sana, furaha na ikiwa ana furaha, mimi pia.”

Fowadi huyo wa Al Hilal, ambaye hatarajiwi kurejea uwanjani hadi Agosti, alihudhuria mashindano ya Formula One Bahrain Grand Prix mwishoni mwa juma lililopita.

Neymar na Messi walishinda mataji ya ligi wakiwa PSG, lakini walishindwa kuleta mafanikio ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa klabu hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, alisema yeye na Messi waliishi kuzimu katika muda wao wa pamoja pale PSG.

Wachezaji wote wawili waliondoka katika klabu hiyo mwaka 2023, huku Messi akijiunga na Ligi Kuu ya Soka ya Marekani (MLS), na Neymar akitia saini mkataba wa miaka miwili na Klabu ya Al Hilal inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudia.

Mfungaji bora wa muda wote wa Brazil, Neymar alionesha nia ya kucheza MLS akiwa PSG.

Alipoulizwa mwaka jana kama angependa kustaafu kuichezea Brazil, Neymar alisema kwenye podikasti ya Fenomenos: “Sijui. Nina shaka kuhusu hilo. Sijui kama nitacheza tena Brazil.

“Ningependa kucheza Marekani, kwa kweli. Ningependa kucheza huko angalau kwa msimu mmoja.”

Makala: Pomboo anavyoakisi ubinadamu kwa Walimwengu
Real Madrid waikataa kadi nyekundu