Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki, limeamua kwa pamoja kumtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uchumi kwa kutambua Uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini Tanzania.

Mageuzi hayo yameboresha ustawi wa Watanzania na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni na yamekuza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.

Hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo itafanyika kesho Alhamis Aprili 18 mwaka 2024, saa sita mchana, katika Chuo Kikuu cha Ankara na ikiongozwa na Prof. Necdet Ünüvar, Mkuu wa Chuo, na kushuhudiwa na Wahadhiri na wanafunzi wa Chuo hicho.

Pia, hafla hiyo itahudhuriwa na Mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao Uturuki.

Akizungumzia tuzo hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema baada ya tukio hilo, Rais Samia ataelekea katika Ikulu ya Uturuki na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwa mazungumzo rasmi na Dhifa ya Kitaifa.

Baadaye Rais Samia ataelekea jijini Istanbul, mji mkuu wa kibiashara wa nchi ya Uturuki, kwa ajili ya kushiriki kwenye Kongamano la kibiashara la Tanzania na Uturuki ambalo litahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Uturuki.

Kalvin Phillips kurudishwa Leeds United
Ten Hag, Garnacho waachiwa msala Man Utd