Swaum Katambo, Tanganyika.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi imeanza maandalizi ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kupanda miche 1,050 ya miti aina mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika.

Akiongoza zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amesema wamepanda miti hiyo ili kuwaenzi waasisi wa Muungano kwa kuwa walipenda kupanda miti mbalimbali huku akiipongeza Halmashauri kwa maandalizi mazuri pamoja na kupanga zoezi la upandaji wa miti lifanyike katika viunga vya Hospitali hiyo kama sehemu ya maadhimisho.

Buswelu amesema licha ya Halmashauri ya Tanganyika kuwa na misitu mikubwa lakini bado wataendelea kupanda miti kwa kuwa shughuli za kibinadamu zinaendelea hivyo kusababisha miti kukatwa.

Awali akitoa taarifa ya zoezi hilo la upandaji miti, Afisa maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bruno Nicolaus amesema aina ya miti iliyopandwa ni Mkangazi na Mkola miti ambayo ipo katika hatari ya kutoweka duniani.

Hata hivyo amesema hadi sasa Halmashauri hiyo imepanda miti zaidi ya milioni mbili kwa mwaka huu.

Halmashauri ya Tanganyika imepanga kuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi kufika Aprili 26 mwaka huu.

Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na Upandaji wa miti, usafi wa mazingira, michezo mbalimbali, dua maalum ya kuliombea Taifa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutembelea wakulima, wafugaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Watakiwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi
Maonesho ya Biashara miaka 60 ya Muungano yafana