Beki na Nahodha wa Liverpool Virgil van Dijk amewataka wachezaji wenzake kusahau yaliyopita ili kujipanga na michezo iliyosalia msimu huu 2023/24.

Wachezaji wa Liverpool walionekana kuwa wanyonge baada ya mchezo wa Ligi kuu ya England dhidi ya Everton uliopigwa usiku wa kuamkia leo katika uwanja wa Goodson Park, ambapo The Reds walikubali kichapo cha 2-0.

Beki huyo kutoka nchini Uholanzi amesema inaumiza kupoteza mchezo huo ambao ulikuwa muhimu kwa Liverpool ambayo inawania Ubingwa msimu huu, lakini hawana budi kukubaliana na uhalisia ili kujipanga na michezo mingine.

“Haikuwa nzuri kwetu, tunapaswa kukubali matokeo haya, ninajua yanaumiza na ndio maana wengi wetu walikuwa wanyonge sana baada ya mchezo, ila tunapaswa kusonga mbele,” Nahodha huyo ameiambia Sky Sports.

“Michezo hii ya mwishoni mwa msimu huwa na changamoto kubwa sana, inapotokea unashinda ni furaha sana, lakini ikiwa tofauti inaweza kupoteza morari kwa wachezaji wa timu nzima, lakini ninapaswa kuwapa moyo wenzangu ili tuendelee kupambana.

“Tulijitahidi kupambana na wapinzani wetu, ninapaswa kukiri walikua vizuri na ndio maana wameshinda kwa idadi ya maboa mawili, na sasa tunapaswa kujipanga na kuwa tayari kwa mechi dhidi ya West Ham United Jumamosi.”

Van Dijk aliendelea: “Kipindi cha pili tulijaribu kulazimisha mambo, na nadhani tulitengeneza nafasi nyingi sana, ninaamini kama tungekuwa makini zaidi ya tulivyokuwa tungeweza kupata zaidi ya mabao matatu. Hata kipindi cha kwanza tulipata nafasi za wazi ambazo tulipaswa kuzitumia na kufunga.

“Lakini hatimaye, hatukuwa wazuri vya kutosha. Hatuwezi kuruhusu msimu kumalizika kama ilivyokuwa usiku wa jana na kipindi cha kwanza dhidi ya Crystal Palace, inakatisha tamaa. Tunapaswa kufanya vizuri zaidi kwa kila maana.” amesema beki huyo

TAKUKURU yaongeza mapato machinjio ya Mtakuja
UNICEF yazigusa Shule zilizoathiriwa na mafuriko Rufiji