Serikali nchini kupitia Wizara ya afya, imetangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg, ulioripotiwa Mkoani Kagera.
Katika taarifa iliyochapishwa na Waziri wa afya Ummy Mwalimu imeeleza kuwa mgonjwa wa mwisho alithibitika kutokuwa tena na maambukizi ya Virusi vya Marburg April 19, 2023.
Amesema, hadi kufikia Mei 31, 2023 Tanzania ilikamilisha siku 42 za uangalizi tangu mgonjwa wa mwisho kupona, kama miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inavyotaka.
“Ninatangaza rasmi kuwa Mlipuko wa Ugonjwa wa Marburg Mkoani Kagera umekwisha rasmi. Tumeweza kuumaliza ugonjwa huu kwa mafanikio makubwa. Kati ya wagonjwa 4 waliokuwa wamelazwa ni mgonjwa mmoja tu (mtoto wa miezi 18) ndie alifariki,” amesema.
Aidha, “Wagonjwa watatu walipona akiwemo Mtumishi wa Afya -Daktari wa Kituo cha Afya Maruku,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo, iliyochapishwa na Waziri Ummy Mwalimu.