Chama kikuu cha upinzani nchini, Democratic Alliance cha Afrika Kusini kimeanzisha hatua ya kisheria kuilazimisha serikali kumkamata Vladimir Putin ikiwa Rais wa Russia iwapo atahudhuria mkutano uliopangwa kufanyika nchini humo.
Afrika ya Kusini, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kidiplomasia tangu mahakama ya kimataifa ya uhalifu -ICC, ilipotoa hati ya kumkamata Putinambaye anatarajiwa kufanya ziara nchini humo kwa ajili ya mkutano wa nchi wanachama wa BRICS mwezi Agosti.
Chama hicho, kimesema kimeanzisha mchakato wa kuwasilisha ombi mahakamani kuhakikisha serikali inamkamata kiongozi huyo wa Russia na kumkabidhi kwa ICC ikiwa Rais Putin atafika nchini Afrika Kusini.
Kiongozi anayehusika na masuala ya sheria kwenye chama cha Democratic Alliance, Glynnis Breytenbach amesema, “hatua hii ya awali ya kwenda mahakamani inalenga kuhakikisha kuwa Afrika Kusini inatekeleza wajibu wake.”
Afrika Kusini ambayo ni mwanachama wa ICC, ina uhusiano wa karibu wa kidiplomasia na Moscow inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa BRICS ambao unajumuisha nchi za Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini.