Kocha wa Everton Carlo Ancelotti, ameadhibiwa kwa kutozwa faini ya Pauni 8,000, kufuatia kukubali kosa la utovu wa nidhamu ambalo lilipelekea kuonyeshwa kadi nyekundu wakati wa mchezo wa ligi ya England dhidi ya Manchester United, mwishoni mwa juma lililopita.

Meneja huyo kutoka Italia, aliadhibiwa na mwamuzi wa mchezo huo Chris Kavanagh, kwa kosa la kupinga maamuzi ya kukataliwa kwa bao lililofungwa na Dominic Calvert-Lewin dakika za lala salama, kabla ya kubainika alikua ameotea (offside).

Adhabu hiyo inamfanya Ancelotti kuwa meneja wa kwanza, kuonyeshwa kadi nyekundu katika ligi ya England msimu huu, ambapo sheria hiyo imeanza kutumiwa duniani kote.

Kufuatia kukubali kosa, mzee huyo wa miaka 60, ameepuka adhabu ya kufungiwa kukaa kwenye benchi la timu yake, katika mchezo ujao wa ligi dhidi ya Chelsea, utakaochezwa jijini London.

Ancelotti aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mchezo dhidi ya Manchester United uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, hakufanya utovu wa nidhamu dhidi ya mwamuzi Kavanagh, lakini alichokifanya ni kulalamikia maamuzi ambayo hayakumridhisha.

Alisema ilikua haki yake kufanya hivyo, kutokana na mwenendo wa bao lililofungwa na Dominic Calvert-Lewin, kuonekana lilikua sahihi na halikupaswa kukataliwa.

Ancelotti alijiunga na Everton Disemba 21 mwaka jana, akitokea nchini kwao Italia alipokua akikinoa kikosi cha SSC Lazio tangu mwaka 2018.

Ancelotti amewahi kuvinoa vikosi vya klabu za Reggiana (1995–1996), Parma (1996–1998), Juventus (1999–2001),  AC Milan (2001–2009), Chelsea (2009–2011 ), Paris Saint-Germain (2011–2013), Real Madrid (2013–2015) na FC Bayern Munich (2016–2017).

TCRA yatangaza kushindanisha tuzo 17 sekta ya mawasiliano
Mama Magufuli atoa zawadi ya Viti mwendo vya watoto