Bodi ya Filamu Tanzania imetoa siku saba kwa Kampuni ya Usambazaji wa Filamu ijulikanayo kama ‘Pamoja Film Company’ kuwasilisha nyaraka za filamu zake ili kukagua na kuhakikisha kama wamefuata sheria na kanuni zinazosimamiwa na bodi hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kampuni hiyo kubainika kukiuka baadhi ya sheria na kanuni za usambazaji zikiwemo za kutowasilisha miswada ya filamu (script) kabla ya kuanza kurekodi, kuzitangaza kazi hizo kwenye mitandao ya kijamii bila ya kuzifikisha Bodi ya Filamu Tanzania Kwa ajili ya ukaguzi pamoja na kufanya kazi za utengenezaji na usambazaji wa filamu bila kibali.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo alipokuwa akiongea na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Lufingo Exaud  kwenye  kikao kilichofanyika ofisini kwake  leo Jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza kuwa kukiuka sheria na kanuni zinazosimamiwa na bodi ni kosa kisheria.

“Natoa siku saba kwa Kampuni hii kuwasilisha miswada ya filamu zake 12 alizozitangaza na kuzisambaza kinyume cha sheria pamoja na kuleta maelezo kwa maandishi ya kujieleza sababu zilizowapelekea kufanya kazi hizo bila kibali kutoka bodi”,alisema Fissoo.

Filamu hizo zilizotolewa na Kampuni hiyo bila kufuata sheria na kanuni ni; Spompompo, Tanga Raha, Buku 10, Jirani Hafugiki, Mke Sahihi, Chanzo, Ahsante, Je Alaumiwe, Mwaka wa Tisa, Nyaraka na Kanya Boya.

Fisoo ameongeza kuwa Bodi imefanya jitihada kubwa kutoa elimu kwa umma kupitia njia za vipeperushi, kuandaa na kushiriki mikutano na makongamano ya kitaifa na kimataifa, kushiriki maonesho na maadhimisho ya kisekta na kitaifa ikiwa na lengo la kuwaelemisha wadau wa filamu kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta hiyo nchini.

Aidha, amewaonya wadau wote wa filamu kuacha kukiuka sheria na kanuni zinazosimamia tasnia ya filamu nchini kwani kufanya hivyo ni kosa kubwa kisheria, “tunawaonya wadau wote kuacha mara moja tabia hii” alimalizia.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni hiyo, Lufingo Exaud amekiri makosa yake na ameahidi kulipa faini za makosa yote, pia ameomba msamaha mbele ya Bodi hiyo na kuapa kuwa hatorudia tena. Kwa kumalizia ameahidi kuwa balozi mzuri wa Bodi ya Filamu Tanzania na yupo tayari kuwapa elimu wadau wengine wa filamu nchini ili waweze kufuata sheria na kanuni zinazoongoza sekta hiyo.

Mbali na kuahidi kushirikiana na bodi hiyo, Lufingo ameusifia utaratibu wa bodi wa kurahisisha upatikanaji wa vibali kwani kwa sasa baada ya kuwasilisha muswada wa filamu kwa ajili ya ukaguzi utapatiwa kibali ndani ya muda wa siku saba za kazi.

 

Lowassa atoa neno kwa Serikali kuhusu shule zinazoungua moto
Mawasiliano Yaboreshwe Dodoma