Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo amemshukia aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kufuatia kauli yake kuwa serikali inawaandama wafanyabiashara waliokuwa wanaunga mkono harakati za wapinzani.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Bulembo aliwataka wapinzani kumuacha rais Magufuli afanye kazi kwani siasa za majukwaani hivi sasa zimekwisha.

Abdallah Bulembo

Abdallah Bulembo

“Wakati wa siasa za majukwaani umekwisha. Rais amepatikana aachwe afanye kazi, na ili afanya kazi yake vizuri ni lazima akusanye kodi na tusianze kudhoofisha kasi na utendaji wake kwa maneno kama haya,” alisema Bulembo.

Kadhalika, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM alimtaka Lowassa kujitokeza hadharani na kutaja majina ya wafanyabiashara hao aliodai wanaandamwa na serikali.

“Tunamtaka ajitokeze na kuwataja kwa majina watu wanaoonewa na kuongezewa kodi kubwa eti kwa sababu ni wafadhili wa Chadema, kauli kama hizi sio nzuri, zinalenga kuibua mgongano kati ya serikali na wafanyabiashara ambao ndio walipakodi,” alisema Bulembo.

Alisisitiza kuwa suala la kulipa kodi halina uhusiano na ufuasi wa chama chochote cha siasa na kwamba suala la kukwepa kulipa kodi halipo katika utendaji wa serikali ya awamu ya tano.

Akiwa katika kanisa la KKKT wilayani Monduli katika ibada maalum ya kuukaribisha mwaka mpya, Lowassa alidai kuwa hivi sasa serikali imeanza kuwaandama wananchi na wafanyabiashara ambao walikuwa wanaunga mkono harakati za upinzani na kuitaka kutenda haki kwa wote.

 

Noti Bandia zawaliza wafanyabiashara msimu wa Christmas
Mchungaji Lwakatare Aigomea Serikali Kuvunja Jumba Lake